200. Haifai kumuomba mwingine yeyote isipokuwa Allaah pekee

Kama ambavo ameamrisha kuombwa amekataza vilevile kuwaomba wengine na kumshirikisha katika maombi. Amesema (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Sehemu zote za kuswalia ni kwa ajili ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[1]

قُلْ إِنَّمَا أَدْعُو رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِهِ أَحَدًا

“Sema: “Hakika si vyenginevyo mimi namuomba Mola wangu pekee na wala simshirikishi na yeyote.”[2]

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚإِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine hana ushahidi wowote juu ya hilo, basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake, kwani hakika hawafaulu makafiri.”[3]

Kwa hivyo haijuzu kumuomba mwingine asiyekuwa Allaah. Yule mwenye kumuomba mwingine asiyekuwa Allaah ni mshirikina. Ni mamoja aliyeombwa ni Malaika, Mtume au walii – kitendo chake ni shirki kubwa kwa hali yoyote:

وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّن يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَن لَّا يَسْتَجِيبُ لَهُ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ وَهُمْ عَن دُعَائِهِمْ غَافِلُونَ وَإِذَا حُشِرَ النَّاسُ كَانُوا لَهُمْ أَعْدَاءً وَكَانُوا بِعِبَادَتِهِمْ كَافِرِينَ

”Ni nani aliyepotea zaidi kuliko yule anayemwomba badala ya Allaah, ambao hatowaitikia mpaka siku ya Qiyaamah nao hawatambui maombi yao. Na [Qiyaamah] watakapokusanywa watu [miungu ya uongo] watakuwa maadui wao na watakuwa kwa ‘ibaadah zao ni wenye kuzikanusha.”[4]

إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ

”Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu, na hata wakisikia, hawatakuitikieni na siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu.”[5]

Amekiita kitendo hicho kuwa ni shirki. Kwa maana nyingine Allaah pekee ndiye anayetakiwa kuombwa. Hakuna mwingine yeyote anatakiwa kuombwa, si katika waliohai au waliokufa, pasi na kujali atakuwa nani.

[1]72:18

[2]72:20

[3]23:117

[4]46:5-6

[5]35:14

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 219-220
  • Imechapishwa: 16/04/2025