20. Watu ambao matangamano yao si yenye kula khasara

18 – Abu Hurayrah amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mbali na wale Malaika wanaoandika matendo ya watu Allaah anao Malaika wanaozunguka ardhini. Wanapowapata watu wanaomdhukuru Allaah (Ta´ala) wanaita: “Njooni katika utashi wenu!” Kisha wanawazunguka. Wanapotawanyika wanapanda mbinguni ambapo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anasema: “Mmewaacha waja wangu wanafanya nini mlipowaacha?” Wanasema: “Tumewaacha wanakuhimidi, wanakutukuza na wanakutaja.” Ndipo aseme: “Kwani wamekwishaniona?” Wanasema: “Hapana.”Aseme: “Vipi lau wangeniona?” Waseme: “Lau wangekuona basi wangekuhimidi, kukutukuza na kukutaja kwa wingi kulikoni.” Aseme: “Kwani wanatafuta nini?” Waseme: “Wanatafuta Pepo.” Aseme: “Wamekwishaiona?” Waseme: “Hapana.” Aseme: “Vipi lau wangeiona?” Waseme: “Wangeiona basi wangelikuwa na bidii zaidi kulikoni.” Aseme: “Wanajilinda kutokamana na nini?” Waseme: “Wanajilinda kutokamana na Moto.” Aseme: “Kwani wamekwishauona?” Waseme: “Hapana.” Aseme: “Vipi wangeuona?” Waseme: “Wangeuona basi wangeukimbia na kujilinda nao zaidi kulikoni.” Ndipo aseme: “Mimi nakushuhudisheni kwamba nimewasamehe.” Waseme: “Wako ambao wameingia kimakosa. Wameingia humo kwa ajili tu ya haja.” Aseme: “Ni watu ambao matangamano yao si yenye kula khasara. Ni watu ambao matangamano yao si yenye kula khasara.”[1]

Ameipokea av al-Bukhaariy na Muslim.

[1] al-Bukhaariy (6408), Muslim (4689) na at-Tirmidhiy (3600).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtasar-ul-´Uluww, uk 90-91
  • Imechapishwa: 12/04/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy