´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 20: Ni yapi maoni yenu juu ya uongozi?

Jibu: Tunaitakidi kuwa uteuzi wa kiongozi ni faradhi kwa baadhi ya waislamu.

Ummah hauwezi kuwa pasi na kiongozi ambaye anautekelezea mambo ya dini na ya dunia, kuulinda na mashambulizi ya washambulizi na kuwasimamishia adhabu wahalifu.

Uongozi hautimii isipokuwa kwa kuwepo utiifu katika wema na si katika maasi. Jihaad ni yenye kuendelea na kila kiongozi mwema na mtenda madhambi. Wanatakiwa kusaidiwa katika ya kheri na kunasihiwa katika ya shari.

MAELEZO

Uongozi ni miongoni mwa mambo ya lazima ambayo watu hawawezi kujitosheleza nayo. Kusipokuwa na uongozi basi hutokea vurugu, yeyote atasema lolote na atafanya lolote. Mpumbavu hatokoma wala mkandamizaji hatochukuliwa hatua isipokuwa kukiwepo uongozi.

Ni lazima kuteua kiongozi ambaye atawaongoza watu dini na dunia yao ambapo atamzuia mpumbavu kutokamana na mchezo, kumzuia mkandamizaji kutokamana na mashambulizi na kuendelea kwake kukandamiza. Kupitia mtawala huyu atatetea damu ya raia wake na mali yao. Matokeo yake watekeleze faradhi za Allaah wakiwa ni wenye amani. Watawala hawa watasimamisha swalah za ijumaa, swalah za mkusanyiko, swalah za ´iyd na nyenginezo. Pia atawaongoza katika hajj, atawasimamia katika mapambano kwenye njia ya Allaah, atawaongoza kwenda kupambana na makafiri, waasi na majambazi.

Kutokana na haya inasemwa kwamba watu hawawezi kujitosheleza kutokamana na mtawala ambaye atawasimamia mambo yao ya kidini, ya kidunia, kuwazuilia mashambulizi ya washambuliaji na kuwasimamishia adhabu wahalifu. Kwa mfano atampiga bakora na kumfukuza mbali na mji mzinzi ambaye hajawahi kuingia katika ndoa, atampiga mawe mzinzi ambaye kishawahi kuingia katika ndoa pale ambapo itathibiti kuwa kweli amezini, atakata mkono wa mwizi, atamuua mwenye kuua na ataamrisha mema na kukataza maovu. Hata hivyo hawezi kuyahakiki hayo mpaka pale ambapo wasaidizi wake watasaidizana naye. Ikiwa wale walioko chini yake sio wenye kumsaidia basi hakuwezi kutimia chochote kama mfano wa kupambana jihaad na makafiri wachupao mpaka, kuzuia fujo na vurugu na majambazi. Kwa sababu lengo la kuwepo uongozi ni utekelezwaji wa mambo haya. Mambo haya yanaweza kufikiwa kutoka kwa mtawala mwadilifu, mjasiri, mwenye hekima na mwenye kutanguliza yale aliyowajibisha Allaah (´Azza wa Jall). Ni mamoja mambo hayo watu wanayaridhia au hawayaridhii. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ

“Enyi walioamini! Muitikieni Allaah na Mtume anapokuiteni katika yale yenye kukuhuisheni.”[1]

Kutokana na Aayah hii tunapata faida kwamba kila ambcho kaamrisha Allaah na Mtume Wake basi ndani yake ndio kuna uhai na kheri.

Hapa hatutozungumzia haki za mtawala juu ya raia wake na haki za raia juu ya mtawala wake.

Tunasumbuliwa na Hizbiyyuun ambao wanafuata mfumo wa Khawaarij wa kisiri. Tunasumbuliwa nao kwelikweli. Hali imefikia kiasi cha kwamba wapo wanaopinga kuwepo nchi yoyote ya Kiislamu au kwamba yeye juu ya shingo yake kuna utiifu kwa mtawala yeyote wa Kiislamu. Mfano hawa na mfano wao wanatakiwa kuchukuliwa hatua.

Ee Allaah! Watengeneze watawala na waongoze katika yale unayoyapenda na kuyaridhia.

[1] 07:24

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 106-108
  • Imechapishwa: 27/10/2021