20. ´Ammaar bin Yaasir alikuwa amejaa imani

90 – Ibn Idriys ametuhadithia, kutoka kwa Burayd bin ´Abdillaah, kutoka kwa Abu Burdah, kutoka kwa Abu Muusa, aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muumini kwa muumini mwenzie ni kama jengo; upande mmoja unautia nguvu mwingine.”[1]

91 – Wakiy´ ametuhadithia, kutoka kwa Sufyaan, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Abu ´Ammaar, kutoka kwa ´Amr bin Shurahbiyl, ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)  amesema:

“´Ammaar amejaa imani mpaka kwenye mifupa yake.”[2]

92 – ´Aththaam bin ´Aliy ametueleza, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Abu Ishaaq, kutoka kwa Haani’ bin Haani’, ambaye amesimulia:

“Wakati tulipokuwa tumeketi kwa ´Aliy (´alayhis-Salaam) aliingia ´Ammaar, ambapo akasema: “Karibu, mzuri na uliyefanywa mzuri! Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: “´Ammaar amejaa imani mpaka kwenye mifupa yake.”

93 – ´Affaan ametuhadithia: Ja´far bin Sulaymaan ametueleza: Zakariyyaa ametueleza: Nimemsikia al-Hasan akisema:

“Imani haihusiani na madai wala kutamani; hakika hapana vyengine imani ni kile kilichothibiti moyoni na kikasadikishwa na matendo.”[3]

[1] Katika ile ya asili imekuja “Burayd bin ´Abdillaah bin Abiy Burdah, kutoka kwa baba yake Abu Muusa”. Masahihisho yamefanywa baada ya “al-Muswannaf” (1/184/12) na Muslim, ambaye ameipokea kupitia njia hiyohiyo na njia nyenginzo. al-Bukhaariy pia ameipokea.

[2] Hadiyth ni Swahiyh. Cheni ya wapokezi ni Swahiyh hata kama kuna Swahabah anayekosekana. ´Amr bin Shurahbiyl alikuwa ni Abu Maysarah al-Hamadaaniy. Abu ´Ammaar alikuwa akiitwa ´Ariyb bin Humayd. Katika ile ya asili alikuwa akiitwa “Abu ´Uthmaan”, lakini mtunzi wa kitabu akalisahihisha baada ya “al-Muswannaf” na katika vyanzo vyengine. al-Haakim (3/392) ameunganisha cheni ya wapokezi wake kupitia kwa Ibn Mahdiy, kutoka kwa Sufyaan, ambaye ameisimulia “kutoka kwa bwana mmoja katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)”. Katika upokezi mwingine amemwita bwana huyo kama ´Abdullaah, bi maana Ibn Mas´uud. Ameisahihisha kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim na ad-Dhahabiy akaafikiana naye, jambo ambalo linahitaji kuangaliwa vyema. Kwa sababu si al-Bukhaariy wala Muslim hawakumpokea Abu ´Ammaar. Hadiyth ni Swahiyh peke yake.

[3] Haya ni maneno ya al-Hasan al-Baswriy na hayakusihi kutoka kwake. Zakariyyaa bin Hakiym al-Habatiy alikuwa ameangamia, kama alivosema adh-Dhahabiy. Wengine katika walioangamia wameipokea kutoka kwa al-Hasan, kutoka kwa Anas, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kitu ambacho nimekizungumzia katika “Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah wal-Mawdhuu´ah” (1098). Huko nimezindua kosa kubwa lililotokea katika kitabu “Ta´luum-us-Swalaah” (uk. 25) cha Muhammad Mahmuud as-Swawwaaf ambapo ameinasibisha Hadiyth kwa Imaam al-Bukhaariy.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 38
  • Imechapishwa: 13/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy