Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

151 – Allaah (Ta´ala) anaziitikia du´aa na kutatua mahitaji.

MAELEZO

Hii ni miongoni mwa sifa za Allaah ya kwamba anamuitikia mwenye kumuomba. Amesema (Subhaanah):

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ

“Watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi niko karibu Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba.”[1]

Allaah (´Azza wa Jall) ameamrisha kumuomba pale aliposema:

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ

“Mola wenu Amesema: “Niombeni, Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari na ‘Ibaadah Yangu, wataingia Motoni hali ya kudhalilika.”[2]

أَمَّن يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ وَيَجْعَلُكُمْ خُلَفَاءَ الْأَرْضِ ۗ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ ۚ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ

“Au nani anayemuitika aliyedhikika anapomwomba na akamuondoshea dhiki na akakufanyeni makhalifa wa ardhi? Je, yuko mungu pamoja na Allaah? Ni machache mno mnayokumbuka.”[3]

Zipo Aayah zingine nyingi zinazoamrisha kuomba du´aa na kumuitikia mwenye kuomba. Hilo ni katika ukarimu, utoaji na ihsani Yake. Anawaamrisha waja Wake kumuomba ili aweze kuwaitikia, licha ya kwamba hawahitajii. Lakini kwa sababu Anajua kuwa wanamuhitaji, ndipo akawaamrisha kumuomba. Imekuja katika Hadiyth:

“Yule asiyemuomba Allaah, basi anamghadhibikia.”[4]

Du´aa ni miongoni mwa aina kubwa kabisa za ´ibaadah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Du´a ndio ´ibaadah.”[5]

[1]2:186

[2]40:60

[3]27:62

[4]at-Tirmidhiy (3373). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “as-Swahiyhah” (2654).

[5]at-Tirmidhiy (3247), Abu Daawuud (1479) na Ibn Maajah (3828).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 218-219
  • Imechapishwa: 16/04/2025