Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

150 – Du´aa ya waliohai na swadaqah zao zinawanufaisha wafu.

MAELEZO

Haya ni masuala yanahusiana na Fiqh, lakini yana mafungamano na ´Aqiydah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapofariki mwanadamu basi matendo yake yote hukatika isipokuwa vitu vitatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu ambayo watu wananufaika kwayo au mtoto mwema anayemuombea du´aa.”[1]

Mja matendo yake yanakatika kwa kufa kwake, isipokuwa yale aliyosababisha kuendelea kwake baada ya kufa kwake. Mfano wake ni swadaqah yenye kuendelea, kama kuweka waqf ya msikiti au masomo. Muda wa kuwa waqf hii inaendelea kunufaisha, basi analipwa thawabu kwayo.

Mfano mwingine ni kama mtu alifunza Fiqh au ´Aqiydah ambapo akawa na wanafunzi; analipwa thawabu ya yale aliyofunza. Vivyo hivyo kama aliandika kitabu kinachowanufaisha watu; thawabu zake zinaendelea. Yote haya ni katika elimu aliyofunza.

Mfano wa tatu ni mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa. Alioa kwa ajili ya kusalimika na machafu na kutafuta kizazi chema. Baadaye akaruzukiwa mtoto mwema ambaye yeye ndiye alikuwa sababu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika vizuri zaidi mlivyokula ni katika yale machumo yenu – na hakika watoto wenu katika machumo yenu.”[2]

Ikiwa mtoto mwema huyu atamuombea mzazi wake baada ya kufa kwake, basi du´aa yake inamfikia. Jambo hilo ni katika matendo yake aliyosababisha yeye na kwa ajili hiyo ananufaika na matendo ya wengine.

[1]Muslim (1631).

[2]Abu Daawuud (3528) na at-Tirmidhiy (1362).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 215-216
  • Imechapishwa: 15/04/2025