Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

148 – Matakwa Yake yameshinda matakwa yote. Mipango Yake imeshinda nguvu zote. Anafanya akitakacho na si mwenye kudhulumu.

149 – Anatakasa kutokamana na kila ovu na kilichoharibika, kila chenye kasoro na mapungufu:

لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ

“Haulizwi kwa yale Anayoyafanya, lakini wao wataulizwa.”[1]

MAELEZO

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

”Hamtotaka isipokuwa atake Allaah, Mola wa walimwengu.”[2]

Amemthibitishia mja matakwa yake, lakini ni yenye kuingia chini ya matakwa ya Allaah. Mja hawezi kutaka isipokuwa kwa matakwa ya Allaah.

Vovyote utakavyofanya katika sababu mbalimbali, ikiwa Allaah hakukukadiria nazo basi hazitokunufaisha kitu. Matendo yote hayatokunufaisha muda wa kuwa Allaah (´Azza wa Jall) hajakukadiria yakunufaishe. Kinachokupasa wewe ni kufanya sababu, lakini kumbuka kuwa Allaah ndiye mwenye kuwafikisha. Wewe umeamrishwa kufanya sababu.

Allaah anafanya akitakacho katika kheri na shari, neema na adhabu. Hata hivyo si mwenye kuwadhulumu waja Wake, kwa sababu anakiweka kila kitu mahali pake stahiki. Anaweka neema na uongofu kwa yule ambaye anayastahiki mambo hayo, na anamnyima uongofu na utiifu ambaye hastahiki mambo hayo. Hata hivyo si mwenye kudhulumu. Hamuadhibu ambaye ni mtiifu na mwenye kutenda mema, hamlipi thawabu mtenda kwa maasi yake. Allaah (Subhaanah) ni mkamilifu katika dhati Yake, mkamilifu katika majina, katika sifa Zake na katika matendo na katika uumbaji Wake.

Hatoulizwa (Subhaanah) juu ya yale anayoyafanya. Kila kitu anakifanya kutokana na hekima na anakiweka mahali pake stahiki. Kuhusu waja wao wataulizwa, kwa sababu ni wenye kukosea na wanayaweka mambo pasipokuwa mahali pake stahiki. Kwa hivyo kuna tofauti kati ya Muumba na viumbe. Hakutokei kasoro katika matendo ya Allaah, tofauti na matendo ya mja; yuko na dhuluma, hasadi, kiburi na mambo mengine yanayopelekea kukosea katika mambo anayoyafanya.

[1]21:23

[2]81:29

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 214-215
  • Imechapishwa: 15/04/2025