Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

144 – Uwezo ambao unapelekea kitendo, kutokana na uongofu ambao haifai kumsifu kwao kiumbe, unakuwa pamoja na kitendo. Lakini kuhusu uongofu kwa njia ya uzima, kuweza, ustadi na usalama, unakuwa kabla ya kitendo na umefungamana na uzungumzishwaji. Ni kama alivosema (Ta´ala):

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[1]

MAELEZO

Kuweza kunarejea katika uwezo wa mtu. Umegawanyika sampuli mbili:

1 – Kuweza kunakohusiana na utuuzima, maamrisho na makatazo.

2 – Kuweza kunakohusiana na mtu kuweza kutenda na kutekeleza.

Kuweza kunakohusiana na utuuzima maana yake ni mtu kuwa na uwezo wa kufanya au kutokufanya jambo fulani. Utuuzima unahusiana na kuweza kwa namna hii. Mtu asiyekuwa na uwezo si mwenye kuwajibishwa. Mfano wa watu hao ni mwendawazimu na mtoto mdogo. Sio watuwazima na kwa ajili hiyo hawawajibishwi na wala hawakatazwi. Lakini mtoto mdogo akifikisha miaka saba basi ameshakuwa na uwezo na kwa ajili hiyo anaamrishwa kuswali kwa njia ya mapendekezo, malezi na kwa lengo la kupewa mazoezi ya kufanya ´ibaadah. Swalah haimuwajibikii isipokuwa mpaka pale atakapobaleghe na hapo ndipo atawajibishwa. Sampuli hii ya uwezo inakuwa kabla ya kitendo.

Kuweza kunakohusiana na utekelezaji kunakuwa pamoja na kitendo. Kwa mfano suala la kuhiji lina uwezo aina mbili. Allaah (Ta´alaa) amesema:

وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا

”Kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo wa kuiendea.”[2]

Kuweza hapa kunahusiana na uwezo. Ni lazima ahiji yule ambaye anaweza. Uwezo wa kuiendea kunakusudiwa akiba na chombo cha usafiri. Yule mwenye kupata vitu viwili hivyo basi analazimika kuhiji, kwa sababu yuko na uwezo. Huu ni uwezo kabla ya kitendo.

Kuhusu kuweza pamoja na kitendo ni kule kuhiji kwenyewe. Pengine mtu asiwe na uwezo kama vile mwenye ugonjwa sugu au mzee. Huyu hana uwezo wa utekelezaji wa kitendo lakini wakati huohuo anao uwezo wa ule utuuzima. Mtu kama huyu bado hajj iko katika dhimma yake.

Mfano mwingine ni swalah; wakati unapoingia wakati wa swalah, inalazimika kwa mtumzima kuswali. Hata hivyo utekelezaji wake wa swalah utategemea na uwezo wake. Mgonjwa ataswali kwa kusimama; asipoweza basi ataswali kwa kuketi chini; asipoweza basi ataswali kwa ubavu. Kwa maana nyingine analazimika kuswali kwa hali yoyote ile, kwa sababu ana uwezo wa kufanya hivo. Uwezo huu unakuwa kabla ya kitendo. Kuhusu kuweza kulikoambatana na kitendo chenyewe, kunaweza kukosekana kabisa kama ambavo kunaweza kupatikana lakini pamoja na kasoro. Kwa hali yoyote atalazimika kuswali kutegemea na uwezo wake:

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.”[3]

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[4]

Kuna tofauti kati ya uwezo sampuli mbili hizo; wa kwanza unahusiana na uzungumzishwaji, kama alivosema (Ta´ala):

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”

Mwingine umefungamana na utekelezaji.

[1] 2:286

[2] 3:97

[3] 64:16

[4] 2:286

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 207-209
  • Imechapishwa: 09/04/2025