Amesema:

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ

“Waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao.”[1]

Imekuja katika Aayah nyingine:

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يُهَاجِرُوا مَا لَكُم مِّن وَلَايَتِهِم مِّن شَيْءٍ حَتَّىٰ يُهَاجِرُوا

”Na wale walioamini na hawakuhajiri, hamna nyinyi jukumu lolote lile la kuwalinda – mpaka wahajiri.”[2]

Kwa yule asiyejua maana yake atazigonganisha.

Kuhusu maneno Yake:

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يُهَاجِرُوا مَا لَكُم مِّن وَلَايَتِهِم مِّن شَيْءٍ حَتَّىٰ يُهَاجِرُوا

”Na wale walioamini na hawakuhajiri, hamna nyinyi jukumu lolote lile la kuwalinda – mpaka wahajiri.”

Kunakusudiwa msiwarithi. Wakati waumini walipohajiri Madiynah, Allaah (´Azza wa Jall) aliamuru kwamba wasirithiane isipokuwa kwa kuhajiri. Ina maana kwamba pindi mtu anapokufa Madiynah pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakati huohuo yuko na jamaa huko Makkah ambao bado hawajahajiri, basi hawarithiani. Vivyo hivyo akifa mtu Makkah na yuko na jamaa aliyehajiri pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi yule aliyehajiri hatomrithi. Hiyo ndio maana ya Aayah:

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يُهَاجِرُوا مَا لَكُم مِّن وَلَايَتِهِم مِّن شَيْءٍ حَتَّىٰ يُهَاجِرُوا

”Na wale walioamini na hawakuhajiri, hamna nyinyi jukumu lolote lile la kuwalinda – mpaka wahajiri.”

Bi maana msiwarithi. Wakati wenye kuhajiri walipokuwa wengi, ndipo Allaah akarejesha jambo la mirathi kwa ndugu na jamaa, ni mamoja wamehajiri au hawakuhajiri. Hukumu hiyo imetajwa katika:

وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ

”Na wenye uhusiano wa kidamu wana haki zaidi [katika kurithiana] wao kwa wao kwa mujibu wa hukumu ya Allaah kuliko [udugu wa] waumini na wale waliohajiri.”[3]

Kuhusu maneno Yake:

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ

“Waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao.”,

kinachokusudiwa ni katika dini. Waumini ni marafiki na wanasimama imara katika dini wao kwa wao. Hii ndio tafsiri ya yale waliyoyatilia mashaka mazanadiki[4].

[1] 9:71

[2] 8:72

[3] 33:6

[4] Ibn ´Aqiyl al-Hanbaliy amesema:

”Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu kinachoitwa ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah wal-Qadariyyah.” (al-Aadaab ash-Shar´iyyah (1/274))

Ibn Taymiyyah amesema:

”Kama alivosema Imaam Ahmad katika kitabu chake ”ar-Radd ´alaaz-Zanaadiqah wal-Jahmiyyah.”  (Tafsiyr Suurat-il-Ikhlaasw, uk. 239)

Ibn Kathiyr amesema:

”… na hivo ndivo alivosema Ahmad bin Hanbal katika kitabu ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/304))

Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

”Amesema waziwazi Ahmad katika kitabu “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah.” (Fath-ul-Baariy (13/598))

  • Mhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 86-88
  • Imechapishwa: 16/04/2024