Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

41 – Allaah ametakasika kutokamana na mipaka, malengo (الغايات), nguzo (الأركان), viungo vya mwili na zana (الأدوات). Hazungukwi na zile panda sita, kama ilivyo kwa viumbe.

MAELEZO

Hapa mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) anachotaka ni kuraddi mapote mawili:

1 – Mujassimah na Mushabbihah ambao wanamsifu Allaah kuwa na kiwiliwili – Allaah ametakasika kutokana na hayo!

2 – Mu´attwilah ambao wanamkanushia Allaah (Ta´ala) kuwa Kwake juu ya viumbe na kwamba ametengana na viumbe Wake. Bali baadhi yao wanatamka wazi ya kwamba yuko kwa dhati Yake ndani ya kila kitu. Hiyo maana yake ni kwamba Allaah amekita ndani ya viumbe Wake na kwamba amezungukwa na zile pande sita na kwamba hayuko juu yao. Ndipo mtunzi wa kitabu akayakanusha hayo kwa maneno yake haya. Hata hivyo wazushi wanaweza kuyatumia kama fursa na wakayapindisha kwa njia ambayo ikapelekea katika kukanusha, kama alivyobainisha mshereheshaji Ibn Abiyl-´Izz al-Hanafiy. Shaykh Muhammad bin Maaniy´ (Rahimahu Allaah) ameyafupisha maneno yake na kusema:

”Makusudio yake ni kuwaraddi Mushabbihah. Hata hivyo maneno haya ni ya kijumla, yasiyo ya wazi na hayatambuliki kwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Ingelikuwa vyema kuwaraddi kwa dalili kutoka ndani ya Qur-aan na Sunnah kuliko kwa istilahi ambazo zinaweza kufahamika kimakosa. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

Aayah hii inawaraddi Mushabbihah pamoja na Mu´attwilah. Kwa ajili hiyo haitakikani kwa yule mwenye kutafuta haki kutilia umuhimu ibara kama hizi. Allaah (Subhaanah) ni Mwenye kusifiwa kwa sifa kamilifu na tukufu. Yeye (Subhaanah) yuko juu ya viumbe Wake, amelingana juu ya ´Arshi Yake, ametukuka kwa dhati Yake, ametengana mbali na viumbe Wake. Hushuka katika usiku kwenye mbingu ya chini na atakuja siku ya Qiyaamah. Sifa zote hizo ni za kihakika na wala hatuzipindishi maana. Hatupindishi maana ya mkono wa Allaah kwamba ni uwezo wala kushuka Kwake kwamba ni kushuka kwa amri Yake. Hatupindishi maana ya sifa yoyote. Bali tunazithibitisha uwepo wake na si namna yake.

Imamu hakuwa mwenye kuhitaji matamshi kama haya ya kijumla, yasiyokuwa wazi na yaliyozuliwa. Angelisema mtu kuwa maneno hayo amepenyezewa lisingelikuwa jambo la kunishangaza kwa ajili ya kumjengea dhana nzuri. Kwa hali yoyote batili ni yenye kuraddiwa kwa mwenye nayo pasi na kujali ni nani. Yule mwenye kusoma wasifu wa at-Twahaawiy na khaswa katika ”Lisaan-ul-Miyzaan” basi ataona kuwa ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa. Hilo ndilo limetufanya kumdhania vizuri katika mambo kama haya aliyokosolewa.”[2]

[1] 42:11

[2] Haashiyah ´alaa al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 33-35

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 33-36
  • Imechapishwa: 22/09/2024