Hapa nitataja mapote matano ambayo yameipekua imani na ambayo sikuyataja mwanzoni mwa kitabu. Nao ni Jahmiyyah, Mu´tazilah, Ibaadhiyyah[1], Swufriyyah[2] na Fadhwliyyah[3].

Jahmiyyah wanasema kuwa imani ni kule kumtambua Allaah kwa moyo ijapo mtu hakushuhudia kwa ulimi, kutambua utume wala chochote katika utekelezaji wa faradhi. Wamejengea hoja juu ya Malaika, kwa sababu Malaika walikuwa waumini kabla Allaah kuwaumba Mitume.

Mu´tazilah wamesema kuwa imani ni kuamini moyoni na kwenye ulimi pamoja na kujiepusha na madhambi makubwa. Yule anayefanya dhambi kubwa basi imani yake inaondoka na hawi kafiri. Kwa hiyo wanamwita fasiki. Kwa maana nyingine sio muumini wala kafiri lakini hata hivyo atataamiliwa kama muumini.

Ibaadhiyyah wanasema kuwa imani ni ule mkusanyiko wa utiifu; yule mwenye kuacha chochote katika ´ibaadah basi anakuwa kafiri aliyekufuru neema na si kafiri kwa njia ya mshirikina. Wamejengea hoja kwa Aayah:

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ بَدَّلُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ كُفْرًا

”Je, huoni wale waliobadilisha neema ya Allaah kwa kufuru… ”?[4]

Swufriyyah wamesema mfano wa hayo juu ya ´ibaadah. Tofauti iliopo kati yao ni katika maasi. Wanachomaanisha ni kwamba madhambi madogo na makubwa yote ni ukafiri na shirki muda wa kuwa mtu hajatubia kwayo maalum.

Fadhwliyyah wamesema mfano wa hayo juu ya ´ibaadah. Tofauti iliopo kati yao ni katika maasi pia. Wanachomaanisha ni kwamba madhambi yote ni kufuru na shirki ni mamoja yamesamehewa au hayakusamehewa. Hoja yao ni kwamba Allaah si mwenye kudhulumu endapo atawaadhibu watu kwayo, kwa sababu amesema:

لَا يَصْلَاهَا إِلَّا الْأَشْقَى الَّذِي كَذَّبَ وَتَوَلَّىٰ

“… hatouingia kuchomeka isipokuwa muovu mkubwa, ambaye amekadhibisha na akakengeukia mbali.”[5]

Mapote haya matatu ya mwisho ni ya Khawaarij licha ya kwamba wamekinzana katika imani. Shiy´ah wameafikiana na mapote mawili katika hayo, Raafidhwah wameafikiana na Mu´tazilah na Zaydiyyah wameafikiana na Ibaadhiyyah.

[1] Unasibisho wa ´Abdullaah bin Ibaadhw aliyejitokeza katika ukhalifah wa Banuu Umayyah kipindi cha khaliyfah Marwaan bin Ahmad.

[2] Wafuasi wa Ziyaad bin al-Aswfar.

[3] Pengine wamenasibishwa na bwana mmoja akiitwa al-Fadhwl katika Khawaarij. Simjui ni nani.

[4] 14:28

[5] 92:15-16

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 100-102
  • Imechapishwa: 04/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naawswir-ud-Diyn al-Albaaniy