Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kumlaani muislamu ni kama kumuua.”[1]

Vilevile amesema:

“Heshima ya mali yake ni kama heshima ya damu yake.”[2]

´Abdullaah amesema:

“Mnywa pombe ni kama mwenye kumwabudia al-Laat na al-´Uzzaa.”[3]

Wakati dhambi inapofananishwa na dhambi nyingine khatari zaidi, wako baadhi wenye kuonelea kuwa zinalingana. Naona kuwa mtazamo huo hauna mashiko yoyote. Allaah ameyafanya baadhi ya madhambi kuwa khatari zaidi kuliko mengine. Amesema:

إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا

“Endapo mtajiepusha na madhambi makubwa mnayokatazwa, basi Tutakufutieni madhambi yenu madogo na tutakuingizeni katika mahali patukufu.”[4]?

Haya yametajwa sana ndani ya Qur-aan na Sunnah na kutarefuka kuyataja hapa. Hata hivyo Allaah ameyakataza yote hayo ingawa anayaona baadhi kuwa ya khatari zaidi kuliko mengine. Ni kama kwamba anasema mwenye kufanya kitu katika maasi haya basi ameungana na watenda maasi. Kila mmoja katika wao anatenda dhambi kwa kiasi cha ukubwa wa dhambi husika, jambo ambalo linapelekea kuitwa mtenda dhambi ijapo baadhi ni wahalifu zaidi kuliko wengine. Yote hayo yanafasiriwa na Hadiyth yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ushahidi wa uwongo unalingana na shirki.” Kisha akasoma:

فَاجْتَنِبُوا الرِّجْسَ مِنَ الْأَوْثَانِ وَاجْتَنِبُوا قَوْلَ الزُّورِ

”Basi jiepusheni na uchafu wa masanamu, na jiepusheni na kauli za uwongo.”[5] [6]

Haya yanabainisha kuwa shirki na ushahidi wa uwongo vinalingana katika makatazo; Allaah ameyakataza yote mawili sehemu moja. Kwa hivyo mawili hayo katika makatazo ni yenye kulingana, tofauti inapokuja katika dhambi yenyewe. Vivyo hivyo kuhusu madhambi mengine yote.

Huoni namna ambavyo mkono wa mwizi unavyokatwa kwa kuiba kisichopungua robo dinari na kwamba anayeiba chini ya hapo hakatwi mkono? Upande wa lugha wote wawili wanaitwa kuwa ni wezi. Wote wawili ni wezi na wametenda dhambi, lakini adhabu zao zinatofautiana kwa kiwango cha dhambi zao.

Vivyo hivyo kuhusu mzinzi bikira na mzinzi ambaye kishawahi kuingia katika ndoa; wote wawili wamemuasi Allaah, lakini mmoja wao dhambi yake ni kubwa na adhabu yake ni yenye kuumiza zaidi kuliko mwingine.

Vilevile kuhusiana na Hadiyth isemayo:

“Kumlaani muislamu ni kama kumuua.”

Wameshirikiana katika maasi wakati walipoyatenda kisha kila mmoja atastahiki adhabu yake husika kwa kiwango cha dhambi yake.

Mfano wa hayo ni Hadiyth isemayo:

“Heshima ya mali yake ni kama heshima ya damu yake.”

Na kadhalika.

Nimeandika kitabu hiki kutokana na pale ilipofikia elimu yangu na yale niyajuayo katika Qur-aan, maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maneno ya wanazuoni baada yake pamoja na lugha ya kiarabu na madhehebu yake. Kwake Allaah ndio nategemea na Yeye ndiye mwenye kutakwa msaada!

[1] Muslim kupitia kwa Thaabit bin adh-Dhwahhaak al-Answaariy (Radhiya Allaahu ´anh).

[2] Hadiyth ni nzuri. Ameipokea ad-Daaraqutwniy na Abu Nu´aym kupitia kwa Ibn Mas´uud, na al-Bazzaar na Abu Ya´laa kupitia kwa Anas. Kuna nyenye kuitilia nguvu kwa Muslim kupitia kwa Jaabir. Tazama kitabu changu ”Hajjat-un-Nabiy” (103).

[3] Hadiyth ni Swahiyh kama maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Sikuiona kama maneno ya ´Abdullaah, bi maana Ibn Mas´uud. al-Haarith bin Abiy Usaamah ameipokea katika ”al-Musnad” na Abu Bakr ash-Shiyraaziy katika ”Sab´atu Majaalis minal-Amaaliy” kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na Ibn Ma´iyn katika ”at-Taariykh”, Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh”, Abu Bakr al-Malhamiy katika ”Majlisayn fiyl-Amaaliy”, Abul-Hasan al-Abnuusiy katika ”al-Fawaaid”, al-Waahidiy katika ”al-Wasiytw” na adh-Dhwiyaa’ al-Maqdisiy katika ”al-Muntaqaa” kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh), kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[4] 4:31

[5] 22:30

[6] Hadiyth ni dhaifu na ameipokea Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, Ibn Maajah na Ahmad. Ni geni kwa mujibu wa at-Tirmidhiy. Kasoro yake ni kutojulikana kwa baadhi ya wapokezi na mkanganyiko. Nimeibainisha katika ”adh-Dhwa´iyfah” (1110).

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 96-100
  • Imechapishwa: 04/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naawswir-ud-Diyn al-Albaaniy