19. Majina ya Mitume yanakumbushia Mitume na tabia zao

3- Majina ya Manabii na Mitume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Wao ndio mabwana wa wanaadamu. Tabia yao ni tabia tukufu zaidi na matendo yao ni matendo matakasifu zaidi. Majina yao yanawakumbushia, sifa zao na hali zao.

Wanachuoni wamekubaliana juu ya kujuzu kwa hilo[1]. Imepokelewa kutoka kwa kiongozi wa waumini ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba aliandika:

“Usimpe yeyote jina la Mtume.”[2]

Makatazo yake haya ilikuwa ni kwa sababu jina lisitwezwe na kukejeliwa. Hata hivyo imepokelewa ya kwamba alijirudi katika maoni hayo, kama alivyothibitisha hilo Haafidhw Ibn Hajar (Rahimahu Allaah).

Katika kizazi cha kwanza walikuwepo wengi waliokuwa na majina ya Mitume. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpa mtoto wake wa kiume jina la “Ibraahiym” na akasema:

“Jana usiku nimepata mtoto wa kiume na nimempa jina la baba yangu Ibraahiym.”

Ameipokea Muslim.

Jina hilo hilo ndilo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpa mtoto wa kiume mkubwa wa Abu Muusa. Yuusuf bin ´Abdillaah bin Salaam (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinipa jina la “Yuusuf”.”

Ameipokea al-Bukhaariy katika “al-Adab al-Mufrad” na at-Tirmidhiy katika “ash-Shamaa-il”. Ibn Hajar amesema:

“Mlolongo wa wapokezi wake ni Swahiyh.”[3]

[1] Tazama “Sharh Swahiyh Muslim” ya an-Nawawiy (8/437) na “Maraatib-ul-Ijmaa´”, uk. 154 ya Ibn Hazm.

[2] Tazama “Fath-ul-Baariy” (01/573).

[3] Tazama “Zaad-ul-Ma´aad” (02/344-348), “Tuhfat-ul-Mawluud”, uk. 136-144, na “Fath-ul-Baariy” (10/571-574).

  • Mhusika: ´Allaamah Bakr bin ´Abdillaah Abu Zayd
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasmiyat-ul-Mawluwd, uk. 17-18
  • Imechapishwa: 18/03/2017