19. Kuchupa mipaka kwa waja wema ndio lililopelekea kukufuru kwa wanaadamu

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لَا تَغْلُوا فِي دِينِكُمْ

“Enyi Ahl-ul-Kitaab! Msipindukie mipaka katika dini yenu.” (an-Nisaa´ 04:171)

2- Imesihi kupokelewa kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesema kuhusiana na maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَقَالُوا لَا تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلَا تَذَرُنَّ وَدًّا وَلَا سُوَاعًا وَلَا يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرًا

”Wakasema: “Msiwaache waungu wenu – na wala msimwache Wadd na wala Suwaa´ na wala Yaghuuth na Ya’uuq na Nasr!” (Nuuh 71:23)

“Haya ni majina ya waja wema katika watu wa Nuuh. Walipokufa shaytwaan aliwapendezea watu wake watengeneze masanamu na kuyaweka mahali ambapo walikuwa wakikaa na kuyapa majina yao. Wakafanya hivyo na hawakuyaabudu mpaka walipofariki watu wale na elimu ikasahaulika, hivy ndipo wakaabudiwa.”

3- Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Wengi katika Salaf wamesema: “Walipokufa wakawa ni wenye kukaa kwa muda mrefu kwenye makaburi yao kisha wakatengeneza masanamu yenye sura zao. Kulipopita muda mrefu ndipo wakaanza kuwaabudu.”

4- ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msipindukie kwangu kama walivyopindukia manaswara kwa ´Iysaa bin Maryam. Hakika mimi ni mja. Hivyo semeni “Mja wa Allaah na Mtume Wake”.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

5- Ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nakutahadharisheni na kupetuka mipaka. Hakika kilichowafanya kuangamia waliokuwa kabla yenu ni kupetuka mipaka.”[2]

6- Muslim amepokea kutoka kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wameangamia waliochupa mipaka.”

Alisema hivyo mara tatu[3].

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu amebainisha sababu iliowapelekea watu wengi kukufuru ni kuchupa mipaka kwa watu wema. Zipo sababu zengine vilevile kama hasadi na ukandamizaji. Kwa ujumla ni kwamba watu hawa waliwapenda Mitume na waja wema sana kiasi cha kwamba wakachupa mipaka kwao na wakakufuru.

1- Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لَا تَغْلُوا فِي دِينِكُمْ

“Enyi Ahl-ul-Kitaab! Msipindukie mipaka katika dini yenu.” (an-Nisaa´ 04:171)

Hapa wanazungumzishwa manaswara na mayahudi, lakini manaswara ni wenye kupindukia zaidi.

Malengo ya mlango huu ni matahadharisho ya kupindukia katika kuwapenda Mitume na waja wema. Kuwapenda kwao ni dini kwa vile Allaah amesema:

لَا تَغْلُوا فِي دِينِكُمْ

“Msipindukie mipaka katika dini yenu.”

Kupenda na kuchukia kwa ajili ya Allaah ni katika dini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Haamini mmoja wenu mpaka Allaah na Mtume Wake wawe ni wenye kupendwa zaidi kwake kuliko mwengine yeyote.”

 Hata hivyo mapenzi haya hayatakiwi kuwa na upindukaji. Mapenzi haya yanatakiwa yawe kwa sampuli ya kuwafuata na kuwatii, sio kuwaasi na kuwaabudu badala ya Allaah. Kadhalika mapenzi ya kuwapenda wanachuoni na waja wema yanatakiwa yawe kwa kuwatakia radhi na kufuata mwenendo wao. Kwa msemo mwingine ni kwamba mapenzi yanatakiwa yawe ya Kishari´ah.

2- Imesihi kupokelewa kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesema kuhusiana na maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَقَالُوا لَا تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلَا تَذَرُنَّ وَدًّا وَلَا سُوَاعًا وَلَا يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرًا

”Wakasema: “Msiwaache waungu wenu – na wala msimwache Wadd na wala Suwaa´ na wala Yaghuuth na Ya’uuq na Nasr!”

“Haya ni majina ya waja wema katika watu wa Nuuh. Walipokufa shaytwaan aliwapendezea watu wake watengeneze masanamu na kuyaweka mahali ambapo walikuwa wakikaa na kuyapa majina yao. Wakafanya hivyo na hawakuyaabudu mpaka walipofariki watu wale na elimu ikasahaulika, hivy ndipo wakaabudiwa.”

Shaytwaan aliwatia wasiwasi watu wa Nuuh ya kutengeneza picha zao ili wawakumbuke katika ´ibaadah. Walipofariki ndipo shaytwaan akawaendea kwa wale waliokuwepo wakati ule na kuwaambia kwamba baba zao walikuwa wakiwaabudu na wakiwaomba uokozi. Ndipo wakawaabudu. Hii ndio sababu iliopelekea katika kuvuka mipaka. Kumewafanya watu kupotea na kuwaangamiza duniani na Aakhirah.

Elimu kusahulika ina maana kwamba ilipotea. Katika upokezi mwingine imekuja kwamba ilifutwa. Elimu ilipotea na wakaja watu wasiojua lolote. Matokeo yake wakatumbukia katika shirki. Katika Hadiyth kuna dalili inayothibitisha juu ya umuhimu wa elimu na kwamba inapiga vita ujinga. Elimu inapoondoka watu wanatumbukia katika batili na ujinga. Ndani yake kuna fadhilah za elimu ya Kishari´ah.

3- Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Wengi katika Salaf wamesema: “Walipokufa wakawa ni wenye kukaa kwa muda mrefu kwenye makaburi yao kisha wakatengeneza masanamu yenye sura zao. Kulipopita muda mrefu ndipo wakaanza kuwaabudu.”

Maneno yake yanaweza kuwa na maana kwamba wale waliotengeneza masanamu yenye sura zao ndio wale waliowaabudu kulipopita muda na hali zikabadilika. Anaweza kuwa anamaanisha vilevile kwamba waliowaabudu ni kizazi kilichokuja baada yao. Bid´ah shari yake ni kubwa kwa yule mwenye kuizua na kwa wale wataokuja baada yake.

4- ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msipindukie kwangu kama walivyopindukia manaswara kwa ´Iysaa bin Maryam. Hakika mimi ni mja. Hivyo semeni “Mja wa Allaah na Mtume Wake”.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anatahadharisha juu ya kusifu kwa kupindukia na kueleza kusikofaa. Mfano wa hayo ni kama mtu kusema kwamba anajua mambo yaliyofichikana au kwamba anaendesha ulimwengu. Anatakiwa kusifiwa kwa mambo yanayotakikana na kwa haki. Mfano wa hayo ni kama vile kusema kwamba yeye ndiye Mtume bora, kiumbe bora, Mtume wa mwisho, mfikishaji wa ujumbe na mfano wa hayo. Miongoni mwa kuvuka mipaka ni yale aliyosema al-Buswayriy kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anatakiwa kusifiwa kwa njia zote isipokuwa tu mtu asisemi kuwa ni mwana wa Allaah. Huu ni ujinga na upotevu. Si Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala mwengine yeyote haifai kumsifu kwa sifa alizopwekeka nazo Allaah pekee. Wakati ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alipopoteza cheni yake akaipata chini ya ngamia. Si Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala yeyote katika Maswahabah wake hakuna aliyejua wapi ilipo. Ni dalili inayoonyesha kuwa hawajui mambo yaliyofichikana isipokuwa tu yale aliyowafunulia Allaah.

5- Ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nakutahadharisheni na kupetuka mipaka. Hakika kilichowafanya kuangamia waliokuwa kabla yenu ni kupetuka mipaka.”

Haya yalisemwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika hajj ya kuaga wakati alipomwamrisha Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kuleta mawe saba. Hadiyth ameipokea Ahmad na baadhi ya waandishi wa Sunan. Cheni ya wapokezi wake ni nzuri na Hadiyth ni Swahiyh.

Kuvuka mipaka na kuongeza. Hivyo katika mazingira haya itahusiana na kuongeza katika dini yale ambayo Allaah hakuyaidhinisha. Ni wajibu kukomeka katika yale yaliyoko katika Qur-aan na Sunnah pasi na kuongeza wala kupunguza. Watu wanapozidisha watatumbukia katika shirki na Bid´ah.

6- Muslim amepokea kutoka kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wameangamia waliochupa mipaka.”

Alisema hivyo mara tatu.

Mwenye kuchupa mipaka ni yule mwenye kupindukia na mwenye kujikakama anayezidisha katika mambo. Kimsingi maana yake ni kujikakama wakati wa kuongea. Hivo ndivyo anavyokuwa mwenye kuvuka mipaka katika mambo. Mtu kama huyu ni mwenye kujikakama. Ni wajibu kwa mtu kuwa kati na kati anapozungumza na katika mambo mengine yote. Si ruhusa kwa mtu yeyote kuzidisha katika dini wala kupunguza. Ni mamoja awe Malaika, raisi, mwanachuoni wala mwengine yeyote.

[1] al-Bukhaariy (3445).

[2] an-Nasaa’iy (3057), Ibn Maajah (3029), Ahmad (1851) na Ibn Hibbaan. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Ibn Maajah” (2455).

[3] Muslim (2670).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 69-71
  • Imechapishwa: 04/10/2018