20. Makatazo ya kuabudu makaburi au kumuabudu Allaah kwenye kaburi la mtu mwema

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Imesihi kupokelewa kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesimulia kwamb Ummah Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alimtajia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kanisa aliyoiona Habashah na namna ilivyokuwa mapicha. Akasema:

“Hao ndio wale ambao wanapofiwa na mtu mwema au mja mwema, basi hujenga juu ya kaburi lake msikiti na huchora ndani yake picha hiyo. Hao ndio viumbe waovu kabisa mbele ya Allaah.”[1]

2- Watu hawa wamekusanya kati ya fitina mbili; fitina ya makaburi na fitina ya masanamu.

3- al-Bukhaariy na Muslim kumepokelewa ya kwamba ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema vilevile:

“Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anataka kufa alikuwa akijifunika kitambara usoni mwake. Anapohisi joto hukifunua na anasema akiwa katika hali hiyo: “Laana ya Allaah iwe juu ya mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni sehemu ya kuswalia.” Mtume akitahadharisha yale waliyokuwa wakiyafanya. Lau sikuchelea hilo basi kaburi lake lingewachwa nje, isipokuwa yeye alikhofia lisije kufanywa kuwa ni mahali pa kuswalia.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

4- Muslim amepokea kupitia kwa Jundub bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kwamba amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kabla ya kufa kwake kwa siku tano akisema:

“Hakika mimi najitakasa kwa Allaah kuwa na kipenzi wa karibu katika nyinyi. Kwani hakika Allaah amenifanya kuwa kipenzi Wake wa karibu kama alivyomfanya Ibraahiym kuwa kipenzi Wake wa karibu. Na lau ningemchukua yeyote katika Ummah wangu kuwa kipenzi wangu wa karibu, basi ningelimfanya Abu Bakr kuwa kipenzi  wangu wa karibu. Tanabahini! Hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa mahali pa kuswalia. Tanabahini! Msiyafanye makaburi kuwa mahali pa kuswalia. Hakika mimi nawakatazeni na hilo.”[3]

Amekataza hilo mwishoni wa uhai wake. Baada ya makatazo haya halafu akamlaani yule mwenye kufanya hivo. Kuswali kwenye makaburi kunaingi katika hayo hata kama hakukujengwa juu yake msikiti. Hii ndio maana ya maneno yake:

“… isipokuwa yeye alikhofia lisije kufanywa kuwa ni mahali pa kuswalia.”

Hakika Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) hawakujenga msikiti pembezoni mwa kaburi lake. Kila sehemu ambayo kunaswaliwa basi kunakuwa kumefanywa msikiti. Bali kila nafasi ambapo kunaswaliwa ndio kunaitwa msikiti. Kama alivyosema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimefanyiwa ardhi yote kuwa msikiti na safi.”[4]

5- Ahmad amepokea kwa cheni ya wapokezi nzuri kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Hakika waovu katika watu ni wale ambao Qiyaamah kitawakuta nao wako hai na wale wenye kuyafanya makaburi kuwa ni mahali pa kuswalia.”[5]

Ameipokea Abu Haatim katika “as-Swahiyh” yake.

MAELEZO

Mlango huu ni mkubwa kama ule uliokuwa kabla yake. Dalili zinazokemea. Ikiwa dalili zimekuja zikikaripia kumuabudu Allaah kwenye makaburi ya waja wema, vipi ikiwa wataabudiwa na wakafanywa kuwa ni waungu badala ya Allaah? Katika hali hii makemeo yanakuwa na nguvu zaidi. Kwa sababu katika hali ya kwanza kitendo kinapelekea katika shirki na katika hali ya pili kitendo chenyewe ni shirki kubwa.

1- Imesihi kupokelewa kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesimulia kwamb Ummah Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alimtajia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kanisa aliyoiona Habashah na namna ilivyokuwa mapicha. Akasema:

“Hao ndio wale ambao wanapofiwa na mtu mwema au mja mwema, basi hujenga juu ya kaburi lake msikiti na huchora ndani yake picha hiyo. Hao ndio viumbe waovu kabisa mbele ya Allaah.”

Walipohama kwenda Habashah waliona kanisa likiadhimishwa kwa jina “Kanisa la Maria”.  Ndani yake kulikuwa mapicha na mapambo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hao ndio wale ambao wanapofiwa na mtu mwema… “

Hapa kunabainishwa hali ya manaswara na kwamba ni wenye kuchupa mipaka kwa wafu wao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“… na huchora ndani yake picha hiyo.”

Wanachora picha ya mtu huyo mwema au hata wakati mwingine picha yake mwenyewe na wafuasi wake, kama ilivyokuwa kwa watu wa Nuuh. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hao ndio viumbe waovu kabisa mbele ya Allaah.”

Bi maana hawa wanaofanya kitendo hichi ndio viumbe waovu kabisa, kwa sababu kitendo chao kinapelekea katika shirki. Kwa jumla ni kwamba wanafanya hivo kwa sababu ya I´tiqaad yao ya shirki. Wanayaadhimisha makaburi na kujenga juu yake ili waweze kuyaabudu na kuyaomba uokozi. Kwa ajili hiyo wakawa viumbe waovu kabisa. Mwenye kufanya hivo basi amejifananisha na manaswara na amefanya matendo yao. Yule mwenye kujifananisha na watu basi yeye ni katika wao. Makusudio kwa haya ni kutahadharisha juu ya matendo yao. Ummah umetumbukia katika hayo. Waovu zaidi waliofanya mambo kama hayo ni Raafidhwah waliopindukia kwa watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wao ndio wa mwanzo waliojenga misikiti juu ya makaburi na wakayaabudu badala ya Allaah. Baada ya hapo katika miji mingi ya waislamu wakapatikana watu katika Ahl-us-Sunnah ambao wakawafuata kichwa mchunga. Matokeo yake Ummah ukawafuata makafiri hatua kwa hatua:

2- Watu hawa wamekusanya kati ya fitina mbili; fitina ya makaburi na fitina ya masanamu.

Wameyaadhimisha makaburi na wakatengeneza mapicha. Vivyo hivyo wako watu katika Ummah huu ambao wanajifananisha nao ambao wamefanya hivo. Wamejifananisha na manaswara na watu wa Nuuh.

3- al-Bukhaariy na Muslim kumepokelewa ya kwamba ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema vilevile:

“Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anataka kufa alikuwa akijifunika kitambara usoni mwake. Anapohisi joto hukifunua na anasema akiwa katika hali hiyo: “Laana ya Allaah iwe juu ya mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni sehemu ya kuswalia.” Mtume akitahadharisha yale waliyokuwa wakiyafanya. Lau sikuchelea hilo basi kaburi lake lingewachwa nje, isipokuwa yeye alikhofia lisije kufanywa kuwa ni mahali pa kuswalia.”

Hapa kiumbe mtukufu zaidi anahisi maumivu ya kifo ili aweze kupanda ngazi zaidi na awe ni kiigizo kwa Ummah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Laana ya Allaah iwe juu ya mayahudi na manaswara.”

Ameyasema hayo katika hali nzito kama hii ili kuutahadharisha Ummah wake kutokamana na matendo yao. ´Aaishah amesema:

“Lau sikuchelea hilo basi kaburi lake lingewachwa nje… “

Bi maana al-Baqiy´ pamoja na Maswahabah wake. Amesema:

“… isipokuwa yeye alikhofia lisije kufanywa kuwa ni mahali pa kuswalia.”

Alichelea wasije kuja watu na wakajenga msikiti juu yake baada ya kutoweka Maswahabah. Maswahabah wao hawakufanya hivo. Lakini jambo hilo linafaywa hii leo na baadhi ya watu wajinga. Wanautembelea msikiti na kumuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nyuma ya kuta. Hii ni shirki kubwa.

Hadiyth inaonyesha ghera waliokuwa nayo Maswahabah na pupa yao juu ya Ummah. Kwa ajili hiyo ndio maana wakawanukulia Ummah Hadiyth hizi.

4- Muslim amepokea kupitia kwa Jundub bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kwamba amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kabla ya kufa kwake kwa siku tano akisema:

“Hakika mimi najitakasa kwa Allaah kuwa na kipenzi wa karibu katika nyinyi. Kwani hakika Allaah amenifanya kuwa kipenzi Wake wa karibu kama alivyomfanya Ibraahiym kuwa kipenzi Wake wa karibu. Na lau ningemchukua yeyote katika Ummah wangu kuwa kipenzi wangu wa karibu, basi ningelimfanya Abu Bakr kuwa kipenzi  wangu wa karibu. Tanabahini! Hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa mahali pa kuswalia. Tanabahini! Msiyafanye makaburi kuwa mahali pa kuswalia. Hakika mimi nawakatazeni na hilo.”

Mapenzi haya ni aina ya juu kabisa ya mapenzi. Hadiyth inathibitisha fadhilah za Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) na kwamba yeye ndiye Swahabah bora kwa maafikiano. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Na lau ningemchukua yeyote katika Ummah wangu kuwa kipenzi wangu wa karibu, basi ningelimfanya Abu Bakr kuwa kipenzi  wangu wa karibu.”

Lakini hakufanya hivo kwa sababu mapenzi yake kumpenda yasije kuchanganyikana na mapenzi ya kumpenda Allaah (´Azza wa Jall). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Tanabahini! Hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa mahali pa kuswalia.”

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Tanabahini! Hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Mitume wao na waja wao wema kuwa ni mahali pa kuswalia.”

Tamko limeanguka kwa sababu mtunzi wa kitabu amelinukuu kutoka katika kitabu “Iqtidhwaa´-us-Swiraat al-Mustaqiym” ambapo linakosekana. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kitendo hicho kwa njia tatu:

1- Ameyakemea wayafanyayo.

2- Amesema:

“Msiyafanye… “

3- Amesema:

“Hakika mimi nawakatazeni na hilo.”

Huku ni kutilia mkazo kwa yale anayoyakataza kwa sababu kitendo hicho kinapelekea katika shirki, kama ilivyotokea hii leo. ´Aaishah amesema:

“… isipokuwa yeye alikhofia lisije kufanywa kuwa ni mahali pa kuswalia.”

Kwa sababu kuswali kwenye makaburi ni kuyafanya misikiti. Kila sehemu ambayo kunaweza kuswaliwa ni msikiti. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimefanyiwa ardhi yote kuwa msikiti na safi.”

Mtu akiswali kwenye makaburi basi ameyafanya kuwa msikiti hata kama haukujengwa. Mtu asemeje ikiwa kumejengwa kitu? Ni njia inayopelekea katika shirki.

5- Ahmad amepokea kwa cheni ya wapokezi nzuri kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Hakika waovu katika watu ni wale ambao Qiyaamah kitawakuta nao wako hai na wale wenye kuyafanya makaburi kuwa ni mahali pa kuswalia.”

Ameipokea Abu Haatim katika “as-Swahiyh” yake.

Kwa sababu Qiyaamah hakitowasimamia isipokuwa viumbe waovu kabisa. Kuhusu waumini watakufa kabla ya hapo ambapo kutakuja upepo uzichukue roho zao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“… na wale wenye kuyafanya makaburi kuwa ni mahali pa kuswalia.”

Hawa pia ni katika viumbe waovu kabisa. Kwa sababu wamesababisha watu kutumbukia katika shirki, Bid´ah na batili. Kwa sababu watu wanapoona kaburi limejengwa wanaanza kufikiria kuwa linatakiwa kuombwa na kutakwa msaada.

Hakuna neno kukiwepo msikiti karibu na makaburi. Pamoja na hivyo ukitenganishwa kwa kuwekwa barabara ndio bora zaidi.

[1] al-Bukhaariy (434) na Muslim (528).

[2] al-Bukhaariy (436) na Muslim (531).

[3] Muslim (532).

[4] al-Bukhaariy (335) na Muslim (521).

[5] Ahmad (3844), Ibn Khuzaymah (789), Ibn Hibbaan (6847) na at-Twabaraaniy (10413). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”ath-Thamar al-Mustatwab” (1/363).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 72-75
  • Imechapishwa: 04/10/2018