18. Mlango kuhusu maneno Yake (Ta´ala) ”Hakika wewe huwezi kumwongoza umpendaye”

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ

”Hakika wewe huwezi kumwongoza umpendaye.” (al-Qaswasw 28:56)

2- Imesihi kupokelewa kutoka kwa Ibn-ul-Musayyab ambaye ameeleza kutoka kwa baba yake aliyesimulia:

“Wakati mauti yalipomfikia Abu Twaalib alimjia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na alikuwepo ´Abdullaah bin Abiy Umayyah na Abu Jahl. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Ewe ami yangu! Sema: “Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah”. Ni maneno ambayo nitakutetea kwayo mbele ya Allaah. Wakamwambia: “Hivi kweli unataka kuacha dini ya ´Abdul-Muttwalib?” Akamrudilia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nao wawili wakamrudilia. Mwishowe neno lake la mwisho alilosema ni kwamba yeye yuko katika dini ya ´Abdul-Muttwalib na akakataa kusema kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Nitakuombea msamaha midhali sijakatazwa.” Ndipo Allaah (´Azza wa Jall) akateremsha:

مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَن يَسْتَغْفِرُوا لِلْمُشْرِكِينَ

”Haimpasii Nabii na wale walioamini kuwaombee msamaha washirikina.” (at-Tawbah 09:113)

Allaah akateremsha pia kuhusu Abu Twaalib:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ

”Hakika wewe huwezi kumwongoza umpendaye lakini Allaah ndiye anamwongoza mtakaye.” (al-Qaswasw 28:56)

MAELEZO

Katika mlango huu alichokusudia mtunzi wa kitabu ni kwamba Mitume, akiwemo mbora wao Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhii wa sallam) hawawezi kujiamualia lolote isipokuwa yale aliyowapa Allaah. Wao hawawezi kuwaongoza watu isipokuwa wale walio-ongozwa na Allaah. Wao ni wenye kuongozwa na wako chini ya uendeshaji Wake. Hawawezi kufanya chochote isipokuwa kwa msaada wa Allaah. Kwa ajili hiyo hawasilihi kuabudiwa badala ya Allaah. Wao ni kama watu wengine wote. Lakini hata hivyo Allaah amewafadhilisha kwa ujumbe na unabii. Wao wana ziada ya utukufu, lakini hili haliwafanyi kuwa washirika wa Allaah katika kuendesha ulimwengu, kujua mambo yaliyofichikana, kumwongoza wampendaye na mengineyo. Ikiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuweza kuwaongoza baba zake wadogo Abu Twaalib na Abu Lahab basi hiyo ni dalili inayoonyesha kwamba kuongoka kuko mikononi mwa Allaah. Kwa hivyo ni wajibu kumuomba Yeye (Subhaanah) pekee uongofu. Mlango huu unazungumzia juu ya kwamba uongofu (ambao una maana ya kukubali haki na kuiridhia) hakuna yeyote anayeumiliki isipokuwa Allaah.

Ama uongofu wenye maana ya kuelekeza na kubainisha, uko mikononi mwa Mitume na wafuasi wake katika wanachuoni na walinganizi. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَـٰكِن جَعَلْنَاهُ نُورًا نَّهْدِي بِهِ مَن نَّشَاءُ مِنْ عِبَادِنَا ۚ وَإِنَّكَ لَتَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ

“Lakini Tumeifanya ni nuru tunaongoa kwayo tumtakaye katika waja Wetu; na hakika wewe bila shaka unaongoza kuelekea njia iliyonyooka.” (ash-Shuuraa 42:52)

Bi maana unaelekeza, unaita na kulingania katika njia iliyonyooka. Lakini hata hivyo hawawezi kuziathiri nyoyo ili ziweze kukubali haki. Bali Allaah pekee ndiye anaweza hilo.

2- Imesihi kupokelewa kutoka kwa Ibn-ul-Musayyab ambaye ameeleza kutoka kwa baba yake aliyesimulia:

“Wakati mauti yalipomfikia Abu Twaalib alimjia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na alikuwepo ´Abdullaah bin Abiy Umayyah na Abu Jahl. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Ewe ami yangu! Sema: “Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah”. Ni maneno ambayo nitakutetea kwayo mbele ya Allaah. Wakamwambia: “Hivi kweli unataka kuacha dini ya ´Abdul-Muttwalib?” Akamrudilia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nao wawili wakamrudilia. Mwishowe neno lake la mwisho alilosema ni kwamba yeye yuko katika dini ya ´Abdul-Muttwalib na akakataa kusema kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Nitakuombea msamaha midhali sijakatazwa.” Ndipo Allaah (´Azza wa Jall) akateremsha:

مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَن يَسْتَغْفِرُوا لِلْمُشْرِكِينَ

”Haimpasii Nabii na wale walioamini kuwaombee msamaha washirikina.”

Allaah akateremsha pia kuhusu Abu Twaalib:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ

”Hakika wewe huwezi kumwongoza umpendaye lakini Allaah ndiye anamwongoza mtakaye.”

al-Musayyab pia inaweza kuandikwa al-Musayyib, lakini lililoenea zaidi kwa wanachuoni wa Hadiyth ni al-Musayyab.

Wakati Abu Twaalib kulipoonekana kwake alama za kutaka kukata roho, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwendea kumlingania ulinganizi maalum. Hapo kabla alikuwa ameshamlingani sana. Pamoja na kwamba alijua kuwa ni haki hakukubaliwa kwa madai kwamba eti asije kutukanywa na watu wake.  Kwa ajili hiyo akasema katika mashairi yake:

Nilijua kuwa dini ya Muhammad

ndio dini bora ya viumbe

Isingekuwa kwa ajili ya lawama na kuogopwa kutukanywa

basi ungeniona ni mwenye kufunguka waziwazi na kukubali

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema “Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah”. Ni maneno ambayo nitakutetea kwayo mbele ya Allaah.” Bi maana ningekushuhudilia na kufanya niwezayo kukuokoa.

Wakasema “Hivi kweli unataka kuacha dini ya ´Abdul-Muttwalib?” Bi maana ´ibaadah ya kuabudu mizimu na masanamu.

Hatimaye maneno ya mwisho ikawa kwamba yeye yuko katika dini ya ´Abdul-Muttwalib. Kwa sababu alikuwa alikuwa ameshahukumiwa kwamba atakuwa na mwisho mbaya. Allaah hakutaka kumwongoza kwa sababu ya hekima kubwa. Hivyo akafa katika dini ya watu wake. Ni kweli. Kumekuja Hadiyth Swahiyh zinazosimulia jinsi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona namna anavyozama kwenye Moto ambapo akamuombea na akatumbukizwa kwenye Moto wa afueni ambapo ubongo wake unachemka[1]. Maoni yanayosema kuwa aliingia katika Uislamu hayana msingi wowote.

Hadiyth inathibitisha kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawezi kumwongoza kiumbe yeyote. Aayah:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ

”Hakika wewe huwezi kumwongoza umpendaye lakini Allaah ndiye anamwongoza mtakaye.”

ni liwazo kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waislamu wengine ambao ndugu zao hawakusilimu.

[1] al-Bukhaariy (3883) na Muslim (209).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 67-68
  • Imechapishwa: 04/10/2018