19. Dalili juu ya umilele, ujuzi na hekima ya Allaah

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Amesema (Subhaanah):

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

”Yeye ndiye wa Mwanzo na wa Mwisho na Aliye juu na Aliye karibu, Naye juu ya kila kitu ni Mjuzi.” (57:03)

وَتَوَكَّلْ عَلَى الْحَيِّ الَّذِي لَا يَمُوتُ

”Na mtegemee Aliye hai Ambaye hafi.” (25:58)

وَهُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ

”Naye ndiye Mjuzi, Mwenye hekima.” (66:02)

وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ

“Naye ndiye Mwenye hekima, Mjuzi.” (06:18)

يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا

”Anajua yale yote yanayoingia ardhini na yale yote yanayotoka humo, na yale yote yanayoteremka kutoka mbinguni na yale yote yanayopanda huko.” (34:02)

وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۚ وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ

”Na Kwake pekee zipo funguo za ghaibu; hakuna azijuaye isipokuwa Yeye tu. Na Anajua yale yote yaliyomo barani na baharini. Na halianguki jani lolote ila Hulijua; na wala [haianguki] punje katika viza vya ardhi, na wala [hakianguki] kilichorutubika na wala [hakianguki] kikavu isipokuwa [kimeandikwa] katika Kitabu kinachobainisha.” (06:59)

وَمَا تَحْمِلُ مِنْ أُنثَىٰ وَلَا تَضَعُ إِلَّا بِعِلْمِهِ

“Na mwanamke yeyote yule habebi [mimba] na wala hazai isipokuwa kwa ujuzi Wake.” (35:11)

لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا

”Ili mjue kwamba Allaah juu ya jambo ni Muweza na kwamba Allaah amekwishakizunguka kila kitu kwa ujuzi.” (65:12)

MAELEZO

Aayah hizi Allaah amekusanya ndani yake yale majina Aliyojiita na sifa alizojieleza Mwenyewe baina ya ukanushaji na uthibitisho. Allaah anathibitishiwa sifa kamilifu na anakanushiwa sifa zilizo na mapungufu na kasoro. Tumetangulia kuizungumzia Aayah Kursiy na Suurah “al-Ikhlaasw”. Amesema (Ta´ala):

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

”Yeye ndiye wa Mwanzo na wa Mwisho na Aliye juu na Aliye karibu, Naye juu ya kila kitu ni Mjuzi.”

Amethibitisha (Subhaanah) ya kwamba Yeye ni wa Mwanzo ambaye hakuna kitu kabla Yake. Hivyo ndivyo amesema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ee Allaah! Hakika Wewe ndiye wa Mwanzo na hakuna kitu kabla Yako, Wewe ndiye wa Mwisho na hakuna kitu baada Yako, Wewe ndiye Uliye juu na hakuna kitu juu Yako.”[1]

Aliye juu kwa maana Yeye ndiye Yuko juu ya viumbe vyote. Kwa msemo mwingine hakuna kitu kilicho juu Yake.

Aliye karibu kwa maana hakuna kitu kilicho karibu kuliko Yeye. Kwa msemo mwingine anakijua kila kitu. Hakuna chenye kujificha Kwake.

Kadhalika Aayah nyenginezo baada yake zinazozungumzia juu ya ujuzi na hekima kama vile:

وَهُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ

”Naye ndiye Mjuzi, Mwenye hekima.”

[1] Muslim (2713).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 19/10/2024