Miongoni mwa dalili za Kufufuliwa ni kuwa endapo Allaah (´Azza wa Jall) asingewafufua viumbe na kuwalipa thawabu kwa matendo yao, basi kuwaumba Kwake ingalikuwa mchezo – na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ametakasika kutokana na kufanya mambo kimchezo!

أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لَا تُرْجَعُونَ فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ

“Je, mlidhania kwamba Sisi tulikuumbeni bila kusudio na kwamba nyinyi Kwetu hamtorejeshwa?” Ametukuka Allaah mfalme wa haki [ambaye] hapana mungu wa haki ila Yeye. Mola wa ‘Arshi tukufu.””[1]

Mtu ambaye anayatumia maisha yake kufanya ´ibaadah na utiifu duniani, atakufa na baadaye asifufuliwe? Kafiri ambaye anaeneza maharibifu ardhini na anafanya machafu, atakufa na asifufuliwe? Hilo haliwi kutokana na hekima ya Allaah:

أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ اجْتَرَحُوا السَّيِّئَاتِ أَن نَّجْعَلَهُمْ كَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَوَاءً مَّحْيَاهُمْ وَمَمَاتُهُمْ ۚ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ

“Je, wanadhania wale waliochuma mabaya Tuwafanye wawe sawa na wale walioamini na wakatenda mema na pia sawasawa uhai wao na kufa kwao? – uovu ulioje wanaouhukumu!”[2]

أَفَنَجْعَلُ الْمُسْلِمِينَ كَالْمُجْرِمِينَ مَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ

”Je, Tuwafanye waislamu sawa kama wahalifu? Mna nini nyinyi! Vipi mnahukumu?”[3]

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا بَاطِلًا ۚ ذَٰلِكَ ظَنُّ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ كَفَرُوا مِنَ النَّارِ أَمْ نَجْعَلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَالْمُفْسِدِينَ فِي الْأَرْضِ أَمْ نَجْعَلُ الْمُتَّقِينَ كَالْفُجَّارِ

“Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake pasipo malengo – hiyo ndio dhana ya wale waliokufuru; basi ole wale waliokufuru kwa moto utakaowapata. Je, Tuwajaalie wale walioamini na wakatenda mema kama wenye kueneza ufisadi ardhini au tuwajaalie wachaji kama waovu?”[4]

Pengine muumini asiburudishwe duniani, akaisha maisha ya dhiki na ya tabu – atakufa na asilipwe thawabu za matendo yake mazuri? Kafiri ambaye anaburudika duniani, anawadhulumu wengine na anaeneza maharibifu ardhini, hatolipwa kwa matendo yake? Hili halistahiki kwa hekima ya Allaah (´Azza wa Jall). Kufufuliwa maana yake ni kusimama kutoka ndani ya makaburi:

يَوْمَ يَقُومُ النَّاسُ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ

“… siku ambayo watu watasimama kwa Mola wa walimwengu.”[5]

Wafanyao mazuri na wafanyao mabaya hawatopata malipo yao duniani, malipo yao yanakuwa huko Aakhirah.

[1]23:115-116

[2]45:21

[3]68:35-36

[4]38:27-28

[5]83:6

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 199-200
  • Imechapishwa: 19/01/2025