Kuonyeshwa na kuwakilishwa itakuwa mbele ya Allaah:

يَوْمَئِذٍ تُعْرَضُونَ لَا تَخْفَىٰ مِنكُمْ خَافِيَةٌ

“Siku hiyo mtahudhurishwa, halitofichika tendo lenu lolote lile la siri.”[1]

وَعُرِضُوا عَلَىٰ رَبِّكَ صَفًّا لَّقَدْ جِئْتُمُونَا كَمَا خَلَقْنَاكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ ۚ بَلْ زَعَمْتُمْ أَلَّن نَّجْعَلَ لَكُم مَّوْعِدًا

”Watahudhurishwa mbele ya Mola wako safusafu [huku Allaah atawaambia]: ”Kwa hakika mmetujia kama tulivyokuumbeni mara ya kwanza. Bali mlidai kwamba hatutakuwekeeni miadi hii.”[2]

Watawasilishwa mbele ya Allaah (´Azza wa Jall) hali ya kuwa miguu peku, uchi na pasi na kutahiriwa.

Kisha kutafanywa hesabu ya matendo. Matendo mema na matendo maovu yataonyeshwa na kuwakilishwa. Hili ni kwa muumini peke yake. Ama kafiri hatofanyiwa hesabu kwa njia ya kupimwa kati ya matendo yake mema na maovu, kwa sabab hana matendo mema. Hata hivyo atafanywa kuyakubali madhambi na ukafiri wake.

Wako waumini ambao wataingia Peponi pasi na hesabu. Wengine watafanyiwa hesabu nyepesi – na ni kule kuonyeshwa – ambapo watarudi kwa familia zao hali ya kuwa ni wenye furaha. Wako wengine ambao watahojiwa hesabu. Imekuja katika Hadiyth:

“Atakayehojiwa hesabu, ataadhibiwa.”[3]

Namna hii ndivo ziko ngazi za waumini.

Madaftari yana matendo ya watu waliyoyafanya duniani. Kila mmoja siku ya Qiyaamah atapewa daftari lake. Daftari hilo lina matendo yake aliyoyafanya ulimwenguni. Humo kumeandikwa kila kitu:

وَوُضِعَ الْكِتَابُ فَتَرَى الْمُجْرِمِينَ مُشْفِقِينَ مِمَّا فِيهِ وَيَقُولُونَ يَا وَيْلَتَنَا مَالِ هَـٰذَا الْكِتَابِ لَا يُغَادِرُ صَغِيرَةً وَلَا كَبِيرَةً إِلَّا أَحْصَاهَا ۚ وَوَجَدُوا مَا عَمِلُوا حَاضِرًا ۗ وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا

“Na kitawekwa Kitabu [daftari la rekodi ya vitendo vyote], basi utaona wahalifu ni wenye khofu kwa yale yaliyokuwemo ndani yake na watasema: “Ole wetu! [Tumeangamia]. Kitabu hiki kina nini, hakiachi dogo wala kikubwa isipokuwa kimekidhibiti?” Na watakuta yale [yote] waliyoyatenda yamehudhuria. Na Mola wako Hamdhulumu yeyote.”[4]

وَكُلَّ إِنسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَائِرَهُ فِي عُنُقِهِ ۖ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنشُورًا اقْرَأْ كِتَابَكَ كَفَىٰ بِنَفْسِكَ الْيَوْمَ عَلَيْكَ حَسِيبًا

“Kila mtu Tumemfungia matendo yake shingoni mwake na tutamtolea Siku ya Qiyaamah kitabu akutane nacho hali ya kuwa kimekunjuliwa. [Ataambiwa]: “Soma kitabu chako nafsi yako inakutosheleza leo kukuhesabu.””[5]

فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَيَقُولُ هَاؤُمُ اقْرَءُوا كِتَابِيَهْ إِنِّي ظَنَنتُ أَنِّي مُلَاقٍ حِسَابِيَهْ فَهُوَ فِي عِيشَةٍ رَّاضِيَةٍ فِي جَنَّةٍ عَالِيَةٍ

“Basi ama yule atakayepewa kitabu chake kuliani mwake, atasema: “Hebu chukueni someni kitabu changu. Hakika mimi niliyakinisha kwamba ni mwenye kukutana na hesabu yangu!” Hivyo basi, yeye atakuwa katika maisha ya kuridhisha, kwenye Jannah ya juu.”[6]

Aina ya watu hawa watafurahi watu kuyaona yale yaliyomo ndani ya madaftari yao.

وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِشِمَالِهِ فَيَقُولُ يَا لَيْتَنِي لَمْ أُوتَ كِتَابِيَهْ وَلَمْ أَدْرِ مَا حِسَابِيَهْ يَا لَيْتَهَا كَانَتِ الْقَاضِيَةَ

“Ama yule atakayepewa kitabu chake kushotoni mwake, atasema: “Ee! Laiti nisingepewa kitabu changu na wala nisingelijua hesabu yangu! Ee! Laiti kingelikuwa kifo ndio kumalizika kwangu!”[7]

Atatamani lau asingelifufuliwa na angelikuwa ametokomea tu kwa kifo.

مَا أَغْنَىٰ عَنِّي مَالِيَهْ ۜ هَلَكَ عَنِّي سُلْطَانِيَهْ

“Haikunifaa chochote mali yangu. Madaraka yangu yameniondoka!”[8]

Kugawanywa kwa madaftari itakuwa ima kwa mkono wa kulia au mkono wa kushoto.

[1]69:18

[2]18:48

[3]al-Bukhaariy (6536) na Muslim (2876),

[4]18:49

[5]17:13-14

[6]69:19-22

[7]69:25-27

[8]69:28-29

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 201-202
  • Imechapishwa: 19/01/2025