18. Watoto – pambo la maisha ya dunia na mema yanayobakia

Imepokelewa kwamba Sufyaan ath-Thawriy amesema:

“´Umar bin ´Abdil-´Aziyz alimwambia mwanae ´Abdul-Malik, ambaye alikuwa mgonjwa: “Unajisikiaje?” Akasema: “Kama mwenye kufa.” Akamwambia: “Inapendeza zaidi kwangu uwe katika mizani yangu kuliko mimi kuwa katika mizani yako.” Akamwambia: “Naapa kwa Allaah, ee baba yangu kipenzi! Inanipendeza zaidi kwangu kile unachokipenda kuliko kile ninachokipenda mimi.” Wakati alipofariki mwanawe ´Abdul-Malik, alisema ´Umar: “Ee mwanangu kipenzi! Hakika ulikuwa duniani kama alivosema Allaah (´Azza wa Jall):

الْمَالُ وَالْبَنُونَ زِينَةُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا

“Mali na watoto ni pambo la uhai wa dunia.”[1]

Wewe ulikuwa ni pambo lake bora kabisa. Nataraji hii leo wewe utakuwa miongoni mwa mema yaliyobakia ambayo ndio thawabu bora na matumaini mema zaidi. Naapa kwa Allaah! Inanifurahisha sana mimi kukuita kutoka katika upande wa pili wa nyumba na ukaniitikia.” Baada ya kumzika alisimama kwenye kaburi lake na akasema: “Sikuacha kuendelea kufurahishwa nawe tangu nilipobashiriwa juu yako, lakini hujapatapo kunifurahisha kama hii leo.” Halafu akasema: “Ee Allaah! Msamehe ´Abdul-Malik bin ´Umar na wale wote wanaomuombea msamaha.”[2]

´Abdul-Mubaarak amepokea katika “az-Zuhd”:

“Mwana wa ´Ayaadhw bin ´Uqbah alifariki. Aliposhuka ndani ya kaburi lake, alisema mtu mmoja: “Naapa kwa Allaah! Ikiwa alikuwa mkuu wa jeshi, basi taraji malipo juu yake.” Akasema: “Ni kipi kinachonizuia? Jana alikuwa miongoni mwa mapambo ya dunia, hii leo ni miongoni mwa mema yanayobakia.”[3]

Imepokelewa kuwa mtoto wa hakimu Shurayh aliaga dunia, akamwandaa, akamuosha, akamzika wakati wa usiku na hakuna yeyote aliyejua hilo. Siku ya kufuata akakaa mahakamani. Watu wakaja kama kawaida kumtembelea na kumuuliza juu ya mwanawe. Akasema: “Hivi sasa ameacha kunung´unika na kupata maumivu.” Watu wakafikiria kuwa amepona, ambapo wakafurahishwa na jambo hilo. Ndipo wakasema: “Tunataraji malipo juu yake kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall).” Akacheka, watu wakastaajabishwa na jambo hilo.

Alifariki mtoto wa Wakiy´ bin al-Jarraah, akatoka na kuwasimulia watu Hadiyth arobaini – ziada ya kile alichozowea kukisimulia kila siku.

Abu ´Aliy ar-Raaziy amesema:

“Nilitangamana na al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw (Rahimahu Allaah) kwa miaka thelathini. Sikuwahi kumuona akicheka wala akitabasamu isipokuwa siku ambayo alifariki mwanawe (Rahimahu Allaah). Wakati nilipomuuliza sababu ya kufanya hivo, akajibu: “Allaah (Subhaanah) amelipenda jambo, hivyo nikapenda kile alichokipenda Allaah.”

Ja´far as-Sarraaj amesimulia kutoka kwa Sa´iyd bin ´Uthmaan, ambaye amesema:

“Dhun-Nuun alimtembelea mgonjwa na akaona namna mgonjwa anavyonung´unika. Dhun-Nuun akasema: “Si mkweli katika kumpenda yule asiyesubiri juu ya madhara Yake.” Mgonjwa yule akasema: “Hapana. Wala si mkweli katika kumpenda yule ambaye hakupata ladha juu ya madhara Yake.”

[1] 18:46

[2] ar-Ridhwaa ´an-il-Laah wa Qadhwaa-ih (82-84) ya Ibn Abiyd-Dunyaa.

[3] az-Zuhd (465).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 91-93
  • Imechapishwa: 20/08/2023