Hadiyth ni dalili inayoonyesha kufaa kukatisha swawm inayopendeza na kwamba si lazima kuikamilisha hata pasi na udhuru wowote. Hata hivyo mfungaji anatakiwa kuchunga manufaa ima katika kuendeleza swawm yake au kuikatisha. Ikiwa katika kuikatisha kuna manufaa afungue, kama ambavyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyofungua swawm alipopata chakula kinachomsaidia katika kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Mifano mingine mtu akajiliwa na mgeni, ndugu yake muislamu akamwalika kwenye karamu na maslahi yakahitaji afungue swawm yake. Lakini ikiwa hakuna maslahi yoyote, basi ni bora aendelee na swawm yake. Umm Haaniy´ (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anayefunga swawm ya kujitolea ni kiongozi wa nafsi yake; akitaka anaweza kufunga na akitaka anaweza kufungua.”[1]

an-Nasaa’iy amepokea Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) iliyotajwa katika mlango huu kwa nyongeza isemayo:

“Kwa hakika mfano wa swawm ya mwenye kujitolea ni kama mtu anayetoa swadaqah kutoka katika mali yake; akitaka anaweza kuendeleza nayo na akitaka anaweza kuizuia.”[2]

Hata hivyo nyongeza hii inaonekana haijahifadhiwa ipasavyo, kwani imekuja kwa Muslim kuwa ni maneno ya Mujahid baada ya Hadiyth ya mlango huu.

Maoni yanayosema kuwa inafaa kukatisha swawm ya kujitolea na kwamba si lazima kuilipa ndio madhehebu ya Ahmad, ash-Shaafi´iy na Ishaaq[3] kwa mujibu wa dalili zilizotangulia.

Lakini an-Nakha´iy, Abu Haniyfah na Maalik wamesema kuwa mtu akianza swawm inayopendeza, basi inakuwa ni wajibu wake kuiendeleza na haifai kuivunja pasi na udhuru wowote. Ikiwa ataivunja bila udhuru wowote, basi ni lazima ailipe. Imepokewa kutoka kwa Maalik kuwa hakuna ulazima wa kuilipa[4]. Wale waliowajibisha kulipa wametumia hoja Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) inayosema:

“Mimi na Hafswah tulikuwa tumefunga. Tukaletewa chakula tukakitamani na hivyo tukakila. Baadaye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaja ambapo Hafswah akasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Sisi tulikuwa tumefunga. Tukaletewa chakula tukakitamani na hivyo tukakila.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Fungeni siku nyingine badala yake.”[5]

Maoni ya kwanza ndiyo yenye nguvu zaidi kwa sababu dalili yake ni yenye nguvu. Kuhusu Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anha) inajibiwa kwa njia mbili:

1 – Hadiyth hii ni dhaifu na wanazuoni wameitia dosari.

2 – Kulipa kunafasiriwa kwa njia ya mapendezo. Hivo ndivo anavosema Ibn-ul-Qayyim. Kwa sababu mbadala wa kitu katika hukumu nyingi za kimsingi huchukua nafasi ya msingi wake na swawm katika msingi wake ilikuwa jambo la khiyari, basi ndivyo ilivyo katika mbadala wake, kwa msemo mwingine katika kulipa – na Allaah (Ta´ala) ndiye mjuzi zaidi.

[1] al-Nasaa’iy katika “al-Kubraa” (03/365) na akataja kwamba imechanganywa. Aidha ameipokea al-Bayhaqiy (04/276). al-Haakim ameisahihisha na adh-Dhahabiy akainyamaazia. Haafidhw al-´Iraaqiy ameona kuwa ni nzuri katika “Takhriyj Ahaadiyth-il-Ihyaa” (02/231). Hata hivyo inayo njia zinazotiana nguvu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Aadaab-iz-Zifaaf”, uk. 84.

[2] “Sunan-un-Nasaa’iy” (04/193).

[3] “al-Mughniy” (06/410) na “al-Majmuu’” (06/392).

[4] “al-Hidaayah” (01/127) na “Bidayaat-ul-Mujtahid” (02/199).

[5] al-Tirmidhiy (735), an-Nasaa’iy katika “al-Kubraa” (03/362 na Ahmad (42/20) kupitia kwa az-Zuhriy, kutoka kwa ´Urwah, kutoka kwa ´Aaishah aliyeisimulia.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/25-26)
  • Imechapishwa: 05/02/2025