´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 18: Ni haki zepi ambazo waislamu wako nazo juu yako?

Jibu: Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ

“Hakika si venginevyo waumini ni ndugu.”[1]

Ni wajibu kuwafanya kama ndugu. Wapendelee kile unachojipendelea juu ya nafsi yako na uwachukilie kile unachojichukilia juu ya nafsi yako. Unatakiwa kujitahidi kiasi na unavyoweza juu ya manufaa yao na kuhakikisha uhusiano wao ni mzuri na kwamba ni wamoja na wakusanyike juu ya haki.

Muislamu ni ndugu wa muislamu mwenzie; hamdhulumu, hamdharau, hamdanganyi na wala hamwaibishi.

Aidha unatakiwa kuwapa haki maalum wenye kukuhusu kama wazazi, jamaa, majirani, marafiki na wafanyakazi wenzio.

MAELEZO

Mafungamano ya kiimani ni yenye nguvu. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao; wanaamrisha mema na wanakataza maovu na wanasimamisha swalah na wanatoa zakaah na wanamtii Allaah na Mtume Wake – hao Allaah atawarehemu. Kwani hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hekima.”[2]

وَالَّذِينَ آمَنُوا مِن بَعْدُ وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا مَعَكُمْ فَأُولَـٰئِكَ مِنكُمْ ۚ وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

”Na wale walioamini baada [ya Hijrah] na wakahajiri na wakapambana jihaad pamoja nanyi, basi hao ni katika nyinyi. Jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe katika Shari´ah ya Allaah. Hakika Allaah ni Mjuzi wa kila kitu.”[3]

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

”Hakika si venginevyo waumini ni ndugu, hivyo basi suluhisheni kati ya ndugu zenu na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa.””

Aayah hizi zinabainisha udugu wa Kiislamu.

Udugu wa Kiislamu ndio kifungamanishi kinachowafungamanisha waislamu pasi na kujali jinsia na nchi zao. Mtu akiwa na dini na mwenye kufuata Sunnah, basi ni lazima kwa nduguze wataamiliane naye mambo ya kiwajibu ya kidugu. Wanamtembelea anapokuwa mgonjwa. Wanamnusuru anapodhulumu. Wanasindikiza jeneza lake anapokufa. Wanamsaidia pindi anapofikwa na msiba. Wanampongeza pindi anapopata neema fulani. Wanampendelea yale wanayojipendelea nafsi zao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msioneane hasadi, msipeane bei ya juu kwa ajili ya bidhaa kwa ajili ya kudanganyana, msichukiane, msipeane mgongo na wala baadhi wasiuze juu ya wengine. Kuweni, waja wa Allaah, ndugu. Muislamu ni ndugu ya muislamu mwegine, hamkoseshi nusura wala hamdharau.” Akaashiria kwenye kifua chake mara tatu na kusema: “Uchaji Allaah ni hapa. Inatosha kuonyesha uovu wa mtu akamdharau nduguye muislamu. Kila muislamu juu ya muislamu mwenzie ni haramu; damu yake, mali yake na heshima yake.”[4]

Haki hizi Allaah ameziwajibisha kwa waja Wake wao kwa wao.

Kuhusu haki maalum kama mfano wa haki za wazazi, ndugu, majirani na wafanya kazi, watu sampuli hii kumepokelewa dalili juu ya haki zao. Allaah amemuwajibishia mtoto kuwatende wema wazazi wawili; baba, mama na wazazi wao. Ametaja haki zao sambamba na haki Yake pale aliposema:

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا

“Mola wako ameamrisha, msiabudu yeyote isipokuwa Yeye pekee. Na [ameamrisha vilevile] kuwatendea wema wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe au wote wawili, basi usiwaambie: “Uff!” na wala usiwakemee, na zungumza nao maneno mazuri.”[5]

Haki za wazazi ndio kubwa zaidi baada ya haki ya Allaah (´Azza wa Jall).

Pia ndugu wana haki zao. Amesema (Ta´ala):

وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ

“Jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe katika Shari´ah ya Allaah.”[6]

Allaah amejaalia kati ya ndugu kurithiana na akathibitisha mirathi yao katika Suurah “an-Nisaa´”. Wazazi wawili na ndugu wana haki ya kupewa matumizi ikiwa ni wahitaji.

Pia majirani wana haki kwa majirani wenzake. Hadiyth imesema:

“Yule ambaye anamwamini Allaah na siku ya Mwisho basi amkirimu jirani yake.”[7]

Haki ya jirani kwa jirani mwenzake ni kutoudhiwa, kusaidiwa pindi anapohitajia msaada na kukopeshwa ikiwa jirani mwenzake anao uwezo. Vivyo hivyo marafiki wote; wanayo haki kutoka kwa mwenzao ya kutekelezewa, kuchungiwa amana na kutofanyiwa usaliti.

Wafanya kazi pia wanayo haki ya kutekelezewa. Ni lazima wapewe mishahara yao. Ni lazima kuwatekelezea haki yao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ni dhuluma kwa mkopeshaji mwenye uwezo kuchelewesha deni lake; anajihalalishia kuvunjwa heshima yake na [kujipelekea katika] adhabu.”[8]

Ni lazima kwa waislamu kutekelezeana haki hizi. Kwa masikitiko makubwa hali ya waislamu ni yenye kusikitisha hii leo.

[1] 49:10

[2] 09:71

[3] 8:75

[4] Muslim (2564).

[5] 17:23

[6] 08:75

[7] al-Bukhaariy (6019) na Muslim (47).

[8] Abu Daawuud (3627) na an-Nasaa’iy pasi na tamko ”Ni dhuluma”. Ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf Sunan Abiy Daawuud”.

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 98-101
  • Imechapishwa: 25/10/2021