84 – Ibn ´Ulayyah ametuhadithia, kutoka kwa al-Hajjaaj bin Abiy ´Uthmaan, kutoka kwa Yahyaa bin Abiy Kathiyr, kutoka kwa Hilaal bin Abiy Maymuunah, kutoka kwa ´Atwaa’, kutoka Mu´aawiyah bin al-Hakam, ambaye amesema:

“Nilikuwa na kondoo kati ya Uhud na al-Jawaaniyyah[1] wanaochungwa na kijakazi wangu. Siku moja akaja mbwa mwitu na akamchukua kondoo kutoka kwake. Mimi ni mwanaadamu wa kawaida ambaye hukasirika kama wanavyokasirika watu wengine. Nikaunyanyua mkono wangu na kumpiga kofi. Nikamwendea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumweleza yaliyopitika. Nikasikitika na kumwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Si nimwache huru?” Akasema: “Mwite.”Nikamwita. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Allaah yuko wapi?”[2] Akajibu: “Juu ya mbingu[3].” Akamuuliza: “Mimi ni nani?” Akajibu: “Wewe ni Mtume wa Allaah.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mwache huru. Kwani hakika ni muumini.”[4]

85 – ´Aliy bin Haashim ametuhadithia, kutoka kwa Ibn Abiy Laylaa, kutoka kwa al-Minhaal, kutoka kwa Sa´iyd bin Jubayr, kutoka kwa Ibn ´Abbaas, na kutoka kwa al-Hakam ambaye amesimulia kwamba:

“Bwana mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: “Hakika mama yangu analazimika kuachia huru mtumwa muumini. Mimi nina mtumwa mweusi na asiyekuwa mwarabu.” Akasema: “Nileteeni naye.” Akasema: “Je, unashuhudia ya kuwa hapana mungu wa haki asiyekuwa Allaah na kwamba mimi ni Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ndio.” Ndipo akasema: “Mwache huru.”[5]

[1] Maeneo mawili kaskazini mwa Madiynah.

[2] Inafahamisha kuwa inafaa kuuliza swali hili kwa lengo la mtihani, tofauti na wanavyofikiri watu wengi. Wangeulizwa swali hilo, basi wasingeweza kujibu kisawasawa. Kwa hivyo hebu wajifunze kupitia Hadiyth hii.

[3] Bi maana juu ya mbingu. Kama vile maneno Yake (Ta´ala):

وَلَأُصَلِّبَنَّكُمْ فِي جُذُوعِ النَّخْلِ

“Nitakusulubuni (فِي) katika mashina ya mitende.” (20:71)

Bi maana juu ya mashina ya mitende. Aayah na Hadiyth zinazofahamisha kuwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) yuko juu ya viumbe Wake ni nyingi kiasi cha kwamba haziwezi kudhibitiwa. adh-Dhahabiy emeandika kitabu kuhusiana na mada hiyo kwa jina ”al-´Uluww lil-´Aliy al-Ghaffaar”, na kimechapishwa. Kabla yake Ibn Qudaamah pia alifanya hivo, lakini kitabu chake hakijachapishwa. Isitoshe jawabu la kijakazi limechukuwa kutoka katika mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ فَإِذَا هِيَ تَمُورُ أَمْ أَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يُرْسِلَ عَلَيْكُمْ حَاصِبًا ۖ فَسَتَعْلَمُونَ كَيْفَ نَذِيرِ

“Je, mnadhani mko katika amani na aliyeko juu mbinguni kwamba hatokudidimizeni ardhini, tahamaki hiyo inatikisika? Au mnadhani mko katika amani na aliyeko juu mbinguni kwamba hatokutumieni tufani ya mawe basi mtajua vipi maonyo Yangu?” (67:16-17)

[4] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Bkhaariy na Muslim. Muslim ameipokea kupitia njia ya mtunzi wa kitabu na nyenginezo. Ahmad pia ameipokea kupitia njia hiyohiyo (5/447-448) na kupitia kwa Ibn Kathiyr. Katika baadhi ya cheni za wapokezi amesimulia wazi.

[5] Cheni ya wapokezi ni dhaifu kwa sababu ya Ibn Abiy Layla. Alikuwa mwanachuoni na mwenye fadhilah, lakini kumbukumbu yake ilikuwa mbaya.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 35-36
  • Imechapishwa: 12/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy