17. Yote isipokuwa khiyana na uwongo

77 – Musw´ab bin al-Muqdaam ametuhadithia: ´Ikrimah bin ´Ammaar ametueleza: Abu Zamiyl ametueleza, kutoka kwa Maalik bin Murthid az-Zamaaniy, kutoka kwa baba yake, ambaye amesimulia kuwa Abu Dharr amesema:

“Nilimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kitu gani kitachomuokoa mja kutokana na Moto. Akasema: “Kumwamini Allaah.” Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah, hakika imani inayo matendo.” Akasema: “Utoe katika yale aliyokuruzuku Allaah, au atoe katika yale ambayo Allaah amemruzuku.”[1]

78 – ´Affaan ametuhadithia: Hammaad bin Zayd ametueleza, kutoka kwa ´Aliy bin Zayd, kutoka kwa Umm Muhammad, ambaye amesema:

“Mtu mmoja alimwambia ´Aaishah: “Imani ni kitu gani?” Akasema: “Nipambanue au kwa jumla tu?” Akasema: “Jibu kwa jumla.” Akasema: “Ambaye anafurahishwa na mazuri yake na akahisi vibaya kwa maovu yake ni muumini.”[2]

79 – Muhammad bin Saabiq ametuhadithia: Israaiyl ametueleza, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Ibraahiym, kutoka kwa ´Alqamah, kutoka kwa ´Abdullaah, aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allâhu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muumini si mwenye kutukana, mwenye kulaani,  mwenye maneno machafu wala mwenye majigambo.”[3]

80 – Yahyaa bin Sa´iyd ametuhadithia, kutoka kwa Sufyaan, kutoka kwa Mansuur, kutoka kwa Maalik bin al-Haarith, kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin Yaziyd, kutoka kwa ´Abdullaah, ambaye amesema:

“Muumini anaweza kubeba tabia zote isipokuwa khiyana na uwongo.”[4]

81 – Yahyaa bin Sa´iyd ametuhadithia, kutoka kwa Sufyaan, kutoka kwa Salamah bin Kuhayl, kutoka kwa Musw´ab bin Sa´d, kutoka kwa Sa´d, ambaye amesema:

“Muumini anaweza kubeba tabia zote isipokuwa khiyana na uwongo.”[5]

82 – Wakiy´ ametuhadithia: al-A´mash ametueleza: Nimehadithia kutoka kwa Abu Umaamah ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muumini anaweza kuingia katika kila kitu isipokuwa khiyana na uwongo.”[6]

83 – Husayn bin ´Aliy ametuhadithia, kutoka kwa Zaaidah, kutoka kwa Hishaam, kutoka kwa al-Hasan, kutoka kwa Abu Muusa, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

“Katika zama za mwisho kutakuwa na mitihani kama kipande cha usiku wenye giza. Mtu atarauka hali ya kuwa ni muumini na ifike jioni hali ya kuwa ni kafiri, au arauke hali ya kuwa ni muumini na ifike jioni hali ya kuwa ni kafiri.”[7]

[1] Cheni ya wapokezi ni dhaifu. adh-Dhahabiy amesema kuwa Murthid az-Zamaaniy hajulikani.

[2] Cheni ya wapokezi ni dhaifu. Ibn Hajar amesema kuwa ´Aliy bin Zayd bin Jud´aan ni mnyonge. Umm Muhammad alikuwa ameolewa na baba yake, Zayd bin Jud´aan, na hajulikani. Lakini maneno yake ´Aaishah “Ambaye anafurahishwa na mazuri yake na akahisi vibaya kwa maovu yake ni muumini” yamesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kupitia kwa ´Umar. Imepokelewa na Ahmad na al-Haakim.

[3] Maneno yake si machafu. Jengine ni kwamba uchafu unayaenea maneno na matendo. Ibn-ul-Athiyr amesema:

“Kila tabia mbaya huzingatiwa ni chafu katika maneno na matendo.” (an-Nihaayah)

Cheni ya wapokezi ni Swahiyh. Kitendo cha baadhi kuidhoofisha hakizingatiwi, kama nilivyolibainisha hilo katika “Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah” (314).

[4] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh. Wapokezi wake  ni waaminifu na ni wanamme wa al-Bukhaariy na Muslim, wote isipokuwa Maalik bin al-Haarith as-Sulamiy ar-Raqqiy. Yeye pia ni mwaminifu. 

[5] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Bukhaariy na Muslim. Abu Ishaaq as-Sabiy´iy ameisimulia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia kwa Masw´ab bin Sa´d. Ameipokea al-Qudhwaa´iy katika “Musnad-ush-Shihaab”. Abu Ishaaq alikuwa mudallis na alichanganyikiwa mwishoni mwa uhai wake. al-Haythamiy amesema:

“Ameipokea al-Bazzaar na Abu Ya´laa. Wanamme wake ni wanamme wa Swahiyh.” (Majma´-uz-Zawaaid (1/92))

Mfano wa hayo yamekuja katika “at-Targhiyb wat-Tarhiyb” (4/28), kwamba:

“ad-Daaraqutwniy ameitaja katika “al-´Ilal”, kama maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kama maneno ya Swahabah yote mawili. Ambacho ni cha sawa zaidi ni kama maneno ya Swahabah.”

[6] Cheni ya wapokezi ni dhaifu kwa sababu ya kutojulikana ambaye al-A´mash amehadithia kutoka kwake. Ahmad (5/252) amepokea mfano wake kwa cheni ya wapokezi wa mtunzi. Ibn Abiy ´Aaswim pia ameipokea kupitia kwa al-A´mash.

[7] Swahiyh. Wanamme wote ni wanamme wa Swahiyh. Vilevile Hadiyth imepokelewa kupitia njia mbili zingine kutoka kwa Abu Muusa. Moja iko kwa Abu Daawuud (4259) na nyingine iko kwa Ahmad (4/408). Isitoshe inatiliwa nguvu na Hadiyth ya Abu Hurayrah iliopo kwa Muslim na Ahmad pamoja na Hadiyth ya Anas, ambayo tayari imekwishatangulia katika kitabu (64).

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 34-35
  • Imechapishwa: 12/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy