16. Mtu wa Shaam na Ibn Mas´uud

76 – Abu Mu´aawiyah ametuhadithia, kutoka kwa Daawuud bin Abiy Hind, kutoka kwa Shihr bin Hawshab, kutoka kwa al-Haarith bin ´Umayrah az-Zubayriy ambaye ameeleza:

“Shaam kulitokea tauni, Mu´aadh akasimama Himsw na kutoa Khutbah kwa kusema: “Tauni hii ni rehema kutoka kwa Mola wetu, du´aa ya Mtume wenu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kifo cha wema wenu kabla yenu. Ee Allaah! Wape familia ya Mu´aadh fungu lililotimia katika hiyo!” Wakati aliposhuka kwenye mimbari akamjia mtu na kusema: “´Abdur-Rahmaan bin Mu´aadh amepatwa.” Akasema: “Sote ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea.” Kisha akaondoka kwenda kwake. Wakati ´Abdur-Rahmaan alipomuona akamwambia: “Ee baba yangu kipenzi!

الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ ۖ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُمْتَرِينَ

”Ni haki kutoka kwa Mola wako, basi kamwe usiwe miongoni mwa wenye kufanya shaka.”[1]

Akasema: “Ee mwanangu kipenzi!

سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ مِنَ الصَّابِرِينَ

”Utanikuta – Allaah akitaka – ni miongoni mwa wenye kusubiri.”[2]

Baada ya mmoja katika familia ya Mu´aadh kufariki akafuatia mmoja baada ya mwingine mpaka yeye Mu´aadh akawa wa mwisho wao kupatwa. Akaja al-Haarith bin ´Umayrah az-Zubayriy kumtembelea, ambapo Mu´aadh akapoteza fahamu. Wakati Mu´aadh alipopata fahamu na kumuona al-Haarith akilia. Mu´aadh akasema: “Unalia nini?” Akasema: “Nalia juu ya elimu itayozikwa pamoja nawe.” Akasema: “Kama kweli wewe unalazimika kutafuta elimu, basi itafute kwa ´Abdullaah bin Mas´uud, ´Uwaymir Abud-Dardaa’ na Salmaan al-Faarisiy. Jihadhari na kosa la mwanachuoni.” Nikasema: “Allaah akutengeneze! Nitalijua vipi?” Akasema: “Hakika haki inayo nuru inayotambulika kwayo.” Mu´aadh – Allaah amrehemu – na al-Haarith akatoka kwenda kwa ´Abdullaah bin Mas´uud huko Kuufah. Alipofika kwenye mlango wake, akakuta kundi la maswahiba wa ´Abdullaah bin Mas´uud waliokuwa wakizungumza. Mwishowe mmoja katika wao akauliza: “Ee mtu wa Shaam! Je, wewe ni muumini?” Akasema: “Ndio.” Wakasema: “Je, wewe ni katika watu wa Peponi?” Akasema: “Mimi nina madhambi na sijui Allaah atayafanya nini. Lau ningejua kuwa nimesamehewa kwayo, basi ningekujuzeni kuwa ni katika watu wa Peponi.” Walipokuwa katika hali hiyo tahamaki akajitokeza ´Abdullaah. Wakasema: “Hushangai na ndugu yetu huyu wa Shaam, anayedai kuwa ni muumini lakini hata hivyo hadai kuwa ni katika wakazi wa Peponi?” ´Abdullaah akasema: “Ningesema kimoja wapo basi kingelifuatia kingine.” al-Haarith akasema: “Sote ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea! Allaah amsifu Mu´aadh!” Akasema: “Mu´aadh ni nani?” Akasema: “Mu´aadh bin Jabal.” Akasema: “Kwa nini?” Akasema: “Alitahadharisha kutokana na kosa la mwanachuoni. Nakuapia kwa Allaah kwamba hili ni kosa kutoka kwako, ee Ibn Mas´uud! Imani ni nini kama sio sisi kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho, Pepo, Moto, kufufuliwa na Njia? Tuko na madhambi na hatujui Allaah atayafanya nini. Lau tungelikuwa tunajua kuwa yamesamehewa, basi tungelisema kuwa ni katika watu wa Peponi.” ´Abdullaah akasema: “Umesema kweli, naapa kwa Allaah! Ni kosa nililofanya. Umesema kweli, naapa kwa Allaah! Ni kosa nililofanya.”[3]

[1] 2:147

[2] 37:102

[3] Cheni ya wapokezi mpaka kwa Ibn Mas´uud ni dhaifu  kwa sababu ya Shihr bin Hawshab, ambaye alikuwa mnyonge kutokana  na makosa yake mengi.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 33-34
  • Imechapishwa: 12/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy