18. Mtume hakufasiri sifa za Allaah

76- Kutokana na tuliyoyasema inapata kubainika kwamba hakuna mwingine anayejua uhalisia wa tafsiri wa yale maandiko yasiyokuwa wazi isipokuwa Allaah (Ta´ala) pekee, kwamba wale wenye kupekua uhalisia wake ni katika wapotevu na kwamba haifai kwa yeyote kufanya hivo. Hilo linapelekea yale maandiko yasiyokuwa wazi ndio yaliyofungamana na sifa za Allaah (Ta´ala) na mfano wake na sio yale yanayosemwa kwamba yamekuja kwa njia ya ujumla, yasiyotambulika kwa wale wanachuoni wahakiki au herufi zake ni zenye kukatikakatika. Kwa sababu baadhi ya wanachuoni wana elimu juu ya hayo yaliyotajwa. Kwa mfano Ibn ´Abbaas na wengineo walizungumzia baadhi ya maudhui haya. Kwa hivyo Aayah haihusiani nazo na Allaah ndiye mwenye kujua zaidi.

77- Katika Sunnah imekuja kwa njia mbili:

1- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mambo maovu kabisa ni yale yaliyozuliwa.”[1]

Tafsiri hizi ni katika mambo yaliyozuliwa kwa sababu hazikuwepo wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala wakati wa Maswahabah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nakutahadharini na mambo yaliyozuliwa, kwani kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila ni upotevu”

“Mwenye kusema juu ya Qur-aan kwa maoni yake mwenyewe basi amekosea japokuwa atapatia.”[2]

 Msemo huu juu ya Qur-aan ni maoni yao wenyewe. Amesema vilevile (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mayahudi waligawanyika mapote sabini na moja. Manaswara waligawanyika mapote sabini na mbili. Na Ummah wangu utakuja kugawanyika mapote sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja.” Kukasemwa: “Ni lipi hilo, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni lile litakalofuata kile ninachofuata mimi hii leo na Maswahabah zangu.”

Ameeleza kwamba mengine yote yataingia Motoni. Amesema vilevile (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayezua katika amri yetu kisichokuwemo basi atarudishiwa.”

Tafsiri hizi sio katika dini yake.

2- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisoma Aayah hizi, akaelezea Hadiyth, akawafikishia Maswahabah wake na akawaamrisha wawafikishie wengine pasi na kuzifasiri wala kuelezea juu ya tafsiri yazo. Haijuzu kuchelewesha ubainifu wakati unapohitajika kwa maafikiano. Kama yangelikuwa na tafsiri basi ingelilazimika kubainisha na isingefaa kwake kuchelewesha. Jengine ni kwamba wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliponyamazia hayo basi ililazimika na sisi kumfuata katika jambo hilo, kwani Allaah ametuamrisha kumfuata yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akatueleza kwamba yeye ni kiigizo chema kwetu:

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

“Hakika mna kigezo chema kwa Mtume wa Allaah kwa yule mwenye kumtaraji Allaah na siku ya Mwisho na akamtaja Allaah kwa wingi.”[3]

Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yuko juu ya njia ya Allaah iliyonyooka na yule mwenye kufuata njia yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi bila shaka yuko juu ya njia ya Allaah iliyonyooka. Si vyenginevyo ni wajibu kwetu kumfuata na kusimama pale aliposimama na kunyamazia yale aliyonyamazia ili kupita juu ya njia yake. Njia yake ni yale yote ambayo Allaah ametuamrisha kufuata pale aliposema:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ

“Kwamba hii ni njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuatenei.”

Sambamba na hilo Akatukataza kufuata vijia vyenginevyo na akasema:

وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

“… na wala msifuate njia za vichochoro nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake.” [4]

[1] Muslim (592), Ahmad (3/310) na al-Bayhaqiy (3/313).

[2] Abu Daawuud (3652) na at-Tirmidhiy (2952) ambaye amesema:

”Hadiyth ni geni. Baadhi ya wanachuoni wamemzungumzia Suhayl bin Abiy Hazm.”

[3] 33:21

[4] 06:153

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ut-Ta’wiyl, uk. 35-37
  • Imechapishwa: 19/12/2018