Kumepokelewa maandiko mengi kutoka katika Qur-aan, Sunnah, maneno ya Maswahabah na Taabi´uun juu ya mahimizo ya kuitendea kazi Sunnah na masisitizo ya kushikamana nazo. Miongoni mwa Hadiyth zilizotangaa zaidi ni ile ya al-´Irbaadhw bin Saariyah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituwaidhi mawaidha ambayo nyoyo ziliingiwa na khofu kwayo na macho yakatokwa na machozi. Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni kana kwamba ni mawaidha ya kutuaga, hivyo basi tuusie.” Akasema: “Nimekuacheni juu ya weupe ambao usiku wake ni kama mchana wake; hatopotea nayo isipokuwa mstahiki maangamivu. Hakika yule atakayeishi muda mrefu katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu. Ziumeni kwa magego yenu.”[1]

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Lazimianeni na Sunnah zangu.”

Bi maana njia yangu ambayo mimi nilikuwa juu yake ambayo nimekupambanulieni katika zile hukumu. Ni mamoja hukumu hizo zinahusiana na mambo ya ´Aqiydah, kimatendo, mambo ya lazima au mambo yaliyopendekezwa.

Ama wanachuoni wa misingi kufanya maalum Sunnah ya kwamba ni yale ambayo mtu ametakwa lakini pasi na kutiliwa mkazo, hii ni istilahi iliyozuka baadaye. Walicholenga ni kupambanua kati yake na kati ya faradhi au jambo la wajibu.

Katika Shari´ah neno ´Sunnah` linapotajwa kwa njia ya kuachia kunakusudiwa njia ya kidini ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiifuata katika ´ibaadah zake, miamala yake, tabia yake, kutikisika kwake na kutulizana kwake. ´Urwah bin az-Zubayr (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ala ala Sunnah. Kwani hakika Sunnah ndio nguzo ya dini.”[2]

Bi maana shikamaneni na Sunnah.

Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alikuwa akifuata amri ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), nyayo zake na hali yake na akiyatilia umuhimu kiasi cha kwamba mpaka ikawa inakhofiwa juu ya akili yake kutokana na namna alivyokuwa analitilia umuhimu jambo hilo. Hayo yamepokelewa na Abu Nu´aym na wengineo[3].

az-Zuhriy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Wanachuoni wetu waliotangulia walikuwa wakisema:

“Kushikamana na Sunnah ni uokozi.”[4]

[1] Ibn Maajah (43). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Ibn Maajah” (43).

[2] Ameipokea Muhammad bin Naaswir al-Marwaziy katika ”as-Sunnah”, uk. 34.

[3] Abu Nu´aym katika ”al-Hilyah” (01/310).

[4] ad-Daarimiy katika ”as-Sunnah” yake (01/230) (97) na Abu Nu´aym katika ”al-Hilyah” (03/369).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 49-50
  • Imechapishwa: 12/08/2020