Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Tambua – Allaah akuongoze katika utiifu Wake – kwamba Haniyfiyyah ndio dini ya Ibraahiym; nako ni kule kumuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia Yeye dini. Hilo ndilo Allaah Amewaamrisha watu wote na Amewaumba kwa lengo hilo. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”[1]

Maana ya “waniabudu” ni wanipwekeshe. Kubwa Aliloamrisha Allaah ni Tawhiyd, nayo ni kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah. Kubwa Alilokataza Allaah ni Shirki, nako ni kuomba wengine pamoja Naye. nako ni kuomba wengine pamoja Naye. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.”[2]

Ukiambiwa: “Ni misingi ipi mitatu ambayo ni wajibu kwa mtu kuijua?” sema: “Mja kumjua Mola Wake, dini yake na Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

MAELEZO

Bi maana namuomba Allaah akuongoze na kukuwafikisha katika kumtii.

Haniyfiyyah ndio dini ya Ibraahiym. Nayo ni kumwabudu Allaah pamoja na kumtakasia nia. Imeitwa hivo kwa sababu ya kule kujiengua. Kwa sababu ni dini iliyojiengua kutokamana na shirki  na kwenda katika Tawhiyd. Ndio maana ikaitwa mila iliyojiengua kwa sababu imejieungua kutokamana na shirki na kwenda katika Tawhiyd. Kwa nisba ya Tawhiyd ni mila ilionyooka. Na kwa nisba ya shirki mila ya Haniyfah ni yenye kumili kutoka kwayo. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

قُلْ إِنَّنِي هَدَانِي رَبِّي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ دِينًا قِيَمًا مِّلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۚ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Sema: “Hakika mimi ameniongoza Mola wangu kuelekea njia iliyonyooka – dini iliyosimama imara – mila ya Ibraahiym aliyejiengua kutokana na shirki na kuielekea Tawhiyd na hakuwa miongoni mwa washirikina.”[3]

Kwa hivyo mila ya Haniyfiyyah imeitwa hivo kwa sababu imejiengua kutokamana na shirki na kwenda katika Tawhiyd. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Dini inayopendeza zaidi kwa Allaah ni Haniyfiyyah nyepesi.”[4]

Ikhlaasw ni kumwabudu Allaah na usimwabudu mwingine. Usimshirikishe na mwingine. Kwa sababu mshirikina anamwabudu Allaah pia. Washirikina ambao walitumiwa Mtume walikuwa wanaswali, wanafunga, wanatoa swadaqah, wanahiji na wanamtaja Allaah kwa wingi. Hata hivyo walikuwa wanamshirikisha Allaah na wengine, wanamuomba Allaah na wanawaomba wengine, wanamchinjia Allaah na wanawachinjia wengine, wanamuwekea nadhiri Allaah na wanawawekea wengine licha ya kuwa ´ibaadah ni haki ya Allaah pekee. Ni lazima kumtakasia nia Allaah kwa kumwelekea Yeye pasi na mwingine. Hiyo ndio tofauti kati ya dini ya washirikina na dini ya waislamu.

[1] 51:56

[2] 04:36

[3] 06:161

[4] Ameipokea al-Bukhaariy kwa cheni ya wapokezi pungufu (01/23).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 35-36
  • Imechapishwa: 05/02/2023