18. Ambaye hazungumzi hastahiki kuwa mola wala kuabudiwa

Waislamu katika zama za Maswahabah hawakuwa na shaka yoyote juu ya hili. Pindi walipojitokeza Jahmiyyah na wakasema kuwa Qur-aan ni kiumbe na vilevile Mutazilah, Ashaa´irah na vijukuu vyao ndipo Ahl-us-Sunnah wakawaraddi ya kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah na hayakuumbwa na wakabatilisha ´Aqiydah yao. Kukisemwa kuwa Qur-aan imeumbwa ina maana kwamba Allaah hazungumzi. Ambaye hazungumzi hastahiki kuwa mungu. Ibraahiym (´alayhis-Salaam) alisema kumwambia baba yake:

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنكَ شَيْئًا

“Pindi alipomwambia baba yake: “Ee baba yangu! Kwa nini unaabudu vile visivyosikia na visivyoona na visivyokufaa kitu chochote?”” (19:42)

Kitu kisichosikia na kisichoona. Kitu kisichokuwa na uhai wowote. Katika Aayah nyingine:

وَاتَّخَذَ قَوْمُ مُوسَىٰ مِن بَعْدِهِ مِنْ حُلِيِّهِمْ عِجْلًا جَسَدًا لَّهُ خُوَارٌ ۚ أَلَمْ يَرَوْا أَنَّهُ لَا يُكَلِّمُهُمْ وَلَا يَهْدِيهِمْ سَبِيلًا

“Watu wa Muusa walijichukulia baada yake katika mapambo yao ndama – kiwiliwili kilichokuwa na sauti kama ya ng’ombe [wakikiabudu]. Je, hawakuona kwamba yeye [ndama huyo] hawazungumzishi na wala hawaongozi njia?” (07:148)

Hawazungumzishi kwa kuwa ni kitu kisichokuwa na uhai. Ni dalili inayofahamisha kuwa ambaye hazungumzi hawezi kuwa mungu. Kadhalika imekuja katika Aayah nyingine:

فَأَخْرَجَ لَهُمْ عِجْلًا جَسَدًا لَّهُ خُوَارٌ فَقَالُوا هَـٰذَا إِلَـٰهُكُمْ وَإِلَـٰهُ مُوسَىٰ فَنَسِيَ أَفَلَا يَرَوْنَ أَلَّا يَرْجِعُ إِلَيْهِمْ قَوْلًا

“Akawatolea umbo la ndama aliye na sauti. Wakasema: “Huyu ndiye mungu wenu na mungu wa Muusaa, lakini [Muusa] amesahau.” Je, hawaoni kwamba [ndama huyo] hawarudishii kauli…”

Bi maana hawazungumzishi.

وَلَا يَمْلِكُ لَهُمْ ضَرًّا وَلَا نَفْعًا

“… wala hawamiliki kuwadhuru na wala kuwanufaisha?” (20:88-89)

Kwa kifupi ni kwamba ambaye hazungumzi hastahiki kuwa mola wala kuabudiwa. Kuwa kuwa ni mpungufu. Vipi ataweza kuamrisha, kukataza na kuyaendesha mambo ilihali hazungumzi? Huku ni kumfanya Allaah (Jalla wa ´Alaa) kutokuwa muweza. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

قُل لَّوْ كَانَ الْبَحْرُ مِدَادًا لِّكَلِمَاتِ رَبِّي لَنَفِدَ الْبَحْرُ قَبْلَ أَن تَنفَدَ كَلِمَاتُ رَبِّي

“Sema: “Kama bahari ingelikuwa ni wino wa [kuandika] maneno ya Mola wangu, basi ingelikauka bahari kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu.” (18:109)

وَلَوْ أَنَّمَا فِي الْأَرْضِ مِن شَجَرَةٍ أَقْلَامٌ وَالْبَحْرُ يَمُدُّهُ مِن بَعْدِهِ سَبْعَةُ أَبْحُرٍ مَّا نَفِدَتْ كَلِمَاتُ اللَّـهِ

“Lau kama miti yote iliyomo katika ardhi ingalikuwa kalamu na bahari [ikafanywa wino], ikaongezewa juu yake bahari saba [zengine] yasingelimalizika maneno ya Allaah.” (31:27)

Maneno ya Allaah ambayo anaamrisha na anakataza kwayo daima na siku zote. Maneno ya Allaah hayadhibitikiwi na hayawezi kuandikwa na bahari na kalamu zote za ulimwenguni. Halafu Jahmiyyah wanasema kuwa eti maneno ya Allaah yameumbwa? Kusema Allaah kuwa hazungumzi na haamrishi na kukataza ni kumsifu Allaah kutokuwa na uwezo. Isitoshe inapelekea vilevile kusema kuwa Qur-aan sio maneno ya Allaah. Licha na kuwa Qur-aan ndio msingi wa kwanza katika misingi ya dalili. Ikiwa kweli sio maneno ya Allaah ni vipi yatatumiwa kama dalili?

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 68-70
  • Imechapishwa: 31/12/2023