17. Vitabu vyote vya mbinguni ni maneno ya Allaah na hayakuumbwa

Allaah (Jalla wa ´Alaa) katika sifa Zake za kimatendo ni kwamba anazungumza. Kama ambavyo anaumba, anaruzuku, anahuisha na kufisha, anaendesha mambo, anapenda na kutaka (Subhaanahu wa Ta´ala) vilevile anazungumza maneno yanayolingana na utukufu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) kama zilivyo sifa Zake zingine. Anazungumza pindi anapotaka, anachokitaka na namna anayotaka.

Maneno ya Allaah aina yake ni ya kale milele (قديمة النوع), na yanazuka kutegemea na matukio (حادثة الآحاد). Kwa maana nyingine ni kwamba anazungumza anapotaka. Alizungumza kwa Qur-aan wakati wa kuteremka Kwake, anamzungumzisha Jibriyl, alimzungumzisha Muusa na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) usiku alipandishwa mbingu. Kabla ya hapo alimzungumzisha Aadam (´alayhis-Salaam) na atazungumza siku ya Qiyaamah akiwafanyia watu hesabu. Atawazungumzisha waumini Peponi nao watamzungumzisha. Kwa hivyo anazumgumza kwa maneno maneno aina yake ni ya kale milele, na yanazuka kutegemea na matukio.

Vitabu vyote walivyoteremshiwa Mitume vyote ni maneno ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Miongoni mwavyo ni Qur-aan Tukufu ambayo ndio kubwa yavyo na Allaah amejaalia kuwa ndio yenye kuvihukumu. Kwa hivyo Qur-aan ni maneno Yake (Jalla wa ´Alaa) ya kikweli na sio mafumbo (مجازاً). Qur-aan imeteremka kutoka Kwake na haikuumbwa. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Wanayasema haya kwa mdomo mpana.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 68
  • Imechapishwa: 31/12/2023