16. Radd kwa Ashaa´irah kwamba Qur-aan imechukuliwa kutoka Ubao uliohifadhiwa

Ashaa´irah wanasema kuwa imeandikwa kwenye Ubao uliohifadhiwa na kwamba Jibriyl ameichukua kutoka kwenye Ubao uliohifadhiwa na akateremka nayo kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haya ni maneno batili. Jibriyl hakuyachukua kutoka kwenye Ubao uliohifadhiwa. Bali ameyachukua kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall). Ni kweli kwamba yameandikwa kwenye Ubao uliohifadhiwa. Amesema (Ta´ala):

بَلْ هُوَ قُرْآنٌ مَّجِيدٌ فِي لَوْحٍ مَّحْفُوظٍ

“Bali hii ni Qur-aan tukufu [ilio] kwenye Ubao uliohifadhiwa.” (85:21-22)

وَإِنَّهُ فِي أُمِّ الْكِتَابِ لَدَيْنَا لَعَلِيٌّ حَكِيمٌ

“Hakika hii iko katika mama wa Kitabu Kwetu, bila shaka imetukuka, yenye hekima.” (43:04)

Bi maana Qur-aan. Imeandikwa katika Ubao uliohifadhiwa. Hili halina shaka. Lakini hata hivyo Jibriyl hakuyachukua kutoka kwenye Ubao, kama wanavyosema Ashaa´irah, bali aliyachukua kutoka kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Mambo haya yanatakiwa kutambulika kwa kuwa yametajwa katika ´Aqiydah ya Ashaa´irah.

Shaykh Muhammad bin Ibraahiym (Rahimahu Allaah) ameraddi maneno haya katika kitabu kilichochapishwa kilicho pamoja na fataawaa zake kwa jina “Jawaab-ul-Waadhwih al-Mustaqiym fiy Kayfiyyat-in-Nuzuul al-Qur-aan al-Kariym”. Ameraddi na kusambaratisha ´Aqiydah hii. Kwa sababu kusema kwamba yamechukuliwa kutoka katika Ubao uliohifadhiwa ni njia inayopelekea kusema kuwa Allaah ameyaumba kwenye Ubao uliohifadhiwa, kama wanavyosema Jahmiyyah. Haya yamechukuliwa kutoka katika maneno ya Jahmiyyah. Ni maneno batili ambayo ni wajibu kuzinduka nayo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 67-68
  • Imechapishwa: 30/12/2023