15. Mtiririko wa cheni ya Qur-aan

Amesema (Ta´ala):

وَإِنَّهُ لَتَنزِيلُ رَبِّ الْعَالَمِينَ نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الْأَمِينُ عَلَىٰ قَلْبِكَ لِتَكُونَ مِنَ الْمُنذِرِينَ بِلِسَانٍ عَرَبِيٍّ مُّبِينٍ

“Hakika ni uteremsho wa Mola wa walimwengu. Ameiteremsha Roho mwaminifu juu ya moyo wako ili uwe miongoni mwa waonyaji kwa lugha ya kiarabu ilio wazi.” (26:192-195)

Maneno Yake:

وَإِنَّهُ لَتَنزِيلُ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Hakika ni uteremsho wa Mola wa walimwengu.”

Amezungumza kwayo na yameteremka kutoka Kwake (Subhaanahu wa Ta´ala).

نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الْأَمِينُ

“Ameiteremsha roho mwaminifu… “

Naye ni Jibriyl ambaye kazi yake ni kuteremsha Wahy.

عَلَىٰ قَلْبِكَ لِتَكُونَ مِنَ الْمُنذِرِينَ

“… juu ya moyo wako ili uwe miongoni mwa waonyaji… “

Anazungumzishwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ameyapokea kutoka kwa Jibriyl.

بِلِسَانٍ عَرَبِيٍّ مُّبِينٍ

“… kwa lugha ya kiarabu  ilio wazi.”

Lugha ya Qur-aan ni kiarabu. Ndio lugha faswaha zaidi.

Amesema vilevile (Subhaanahu wa Ta´ala):

إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ

“Hakika hii bila shaka ni kauli ya mjumbe mtukufu.” (81:19)

 Bi maana Jibriyl (´alayhis-Salaam).

ذِي قُوَّةٍ عِندَ ذِي الْعَرْشِ

“Mwenye nguvu kwa huyo Mwenye ´Arshi… “

Bi maana Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

مَكِينٍ

“… na mwenye cheo.”

Bi maana Jibriyl (´alayhis-Salaam). Allaah amempa nguvu na cheo na ukaribu Kwake (Jalla wa ´Alaa).

مُطَاعٍ

“Anayetiiwa… “

Malaika wanamtii.

ثَمَّ أَمِينٍ

“… tena muaminifu.”

Ni mwaminifu juu ya Wahy wa Allaah (´Azza wa Jall). Hizi ndio sifa za Jibriyl (´alayhis-Salaam). Ni mwaminifu ambaye hazidishi wala hapunguzi. Anafikisha kama alivyopokea kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall).

Halafu akasema:

وَمَا صَاحِبُكُم

“Na wala huyu mwenzenu… “

Bi maana Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

بِمَجْنُونٍ

“… hana wazimu.”

Kama wanavyosema washirikina. Amemkanushia wendawazimu.

وَلَقَدْ رَآهُ

“Bila shaka alimuona… “

Bi maana alimuona Jibriyl (´alayhis-Salaam) katika umbile lake la kimalaika. Alimuona kwa juu katika upeo Makkah.

بِالْأُفُقِ

“… upeo.” (81:19-23)

Kwa juu. Alimuona kwa macho yake.

Amesema tena (Jalla wa ´Alaa):

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ

“Hakika alimuona katika uteremko mwingine.” (43:13)

Bi maana Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Jibriyl katika umbile lake kwa mara nyingine kwenye mkunazi wa mpaka wa mwisho kabisa usiku aliposafirishwa juu mbinguni. Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Jibriyl katika umbile lake ambalo Allaah amemuumba kwalo mara mbili; mara ya kwanza ilikuwa Makkah na mara nyingine ilikuwa katika ulimwengu wa juu kwenye mkunazi wa mpaka wa mwisho kabisa. Mbali na hizi Jibriyl alikuwa akimjia Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika umbile la mwanaume ambapo amekaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na watu wake. Tahamaki walikuwa wakiona mtu. Kwa sababu hawawezi kumuona katika umbile lake la kimalaika.

Huu ndio mtiririko wa mlolongo wa Qur-aan. Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wameipokea kutoka kwa Muhammad, Muhammad ameipokea kutoka kwa Jibriyl, Jibriyl ameipokea kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall). Kwa hivyo ni maneno ya Allaah. Kuhusu kuinasibisha kwa Malaika:

إنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ

“Hakika hii bila shaka ni kauli ya mjumbe mtukufu.” (81:19)

Vilevile kuinasibisha kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ وَمَا هُوَ بِقَوْلِ شَاعِرٍ

“Hakika hii bila shaka ni kauli ya Mtume mtukufu na sio kauli ya mshairi.” (60:40-41)

Ni unasibisho kwa njia ya kufikisha. Jibriyl na Muhammad (´alayhimaas-Salaam) wote wawili kazi yao ni kufikisha kutoka kwa Allaah. Maneno yananasibishwa kwa yule aliyeanza kuyasema na hayanasibishwi kwa yule mwenye kuyafikisha. Ni jambo lisilowezekana maneno yakawa ya watu watatu. Allaah amekhabarisha kwamba ni maneno Yake. Ameyanasibisha kwa mjumbe wa kimalaika na mjumbe wa kibinaadamu kwa njia ya kufikisha. Kwa hivyo ni maneno ya Allaah ndiye kaanza kuyazungumza na vilevile ni maneno ya Jibriyl na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) kwa njia kuwa wamefikisha kutoka kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa).

Waislamu hawana shaka juu ya hili ya kwamba ni maneno ya Allaah. Yameteremshwa na wala hayakuumbwa. Amesema (Ta´ala):

إِنَّا أَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ

“Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu.” (39:02)

تَنزِيلُ الْكِتَابِ مِنَ اللَّـهِ

“Ni Uteremsho wa Kitabu kutoka kwa Allaah.” (39:01)

مُنَزَّلٌ مِّن رَّبِّكَ بِالْحَقِّ

“Kimeteremshwa kutoka kwa Mola wako kwa haki.” (06:114)

Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameeleza kuwa ni maneno Yake. Amesema (Ta´ala):

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ ث

“Ikiwa mmoja wa washirikina akikuomba umlinde, basi mlinde mpaka asikie maneno ya Allaah.” (09:06)

يُرِيدُونَ أَن يُبَدِّلُوا كَلَامَ اللَّـهِ

“Wanataka kubadilisha maneno ya Allaah.” (48:15)

Ameeleza kuwa ni maneno Yake na kwamba Yeye ndiye Mwenye kuyateremsha.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 64-67
  • Imechapishwa: 30/12/2023