Moyo wa mlinganizi unatakiwa uwe mkunjufu kwa yule anayekwenda kinyume naye khaswa pale atapotambua kwamba yule aliyefanya hivo ni mwenye nia njema na kwamba hakwenda kinyume naye isipokuwa ni kutokana na vile dalili ilivyomdhihirikia. Mtu anatakiwa afanye mazoezi katika mambo haya na asifanye tofauti hizi kuwa ni chimbuko na kufanyiana uadui na kuchukiana. Isipokuwa kama ni mtu ambaye amekwenda kinyume na mkaidi kwa njia ya kwamba amembainishia haki lakini hata hivyo akaendelea kung´ang´ania batili yake. Huyu anatakiwa kutaamiliwa vile anavostahiki katika kuwakimbiza watu na kutadharisha watu mbali naye. Mtu huyu umebaini uadui wake kwa njia ya kwamba amebainishiwa haki lakini hajisalimishi nayo.

Yapo maswala ya matawi ambayo watu wanatofautiana ambayo ukweli wa mambo ni miongoni mwa mambo ambayo Allaah amewafanyia wasaa waja Wake. Nakusudia maswala ambayo hayatokani na misingi ambayo inapelekea kumkufurisha yule anayeonelea kinyume. Hayo ni miongoni mwa mambo ambayo Allaah amewafanyia wasaa waja na akafanya kosa kuwa lenye wasaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Anapohukumu hakimu ambapo akajitahidi  kisha akapatia, basi ana ujira mara mbili. Na akijitahidi kisha akakosea, basi ana ujira mara moja.”

Mujtahid hatoki moja kwa moja nje ya mzunguko wa ujira; ima akapata ujira mara mbili akipatia na ima akapata ujira mara moja akikosea.

Ikiwa hutaki wengine waende kinyume na wewe basi tambua kwamba wengine pia hawataki yeyote aende kinyume nao. Kama ambavo wewe unataka watu wayachukue maneno yako, wale wanaoenda kinyume nawe pia wanataka watu wayachukue maneno yao. Marejeo wakati wa kuzozana ni yale aliyobainisha Allaah (´Azza wa Jall) pale aliposema:

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبِّي عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ أُنِيبُ

”Jambo lolote lile mlilokhitilafiana kwalo, basi hukumu yake ni kwa Allaah. Huyo ndiye Allaah, Mola wangu, Kwake nategemea na Kwake narejea kutubia.”[1]

Vilevile amesema (´Azza wa Jall):

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[2]

[1] 42:10

[2] 04:59

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Zaad Daa´iyah ila Allaah, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 08/11/2021