18. Kurudi katika Qur-aan na Sunnah na kuacha mizozo

Kwa hivyo ni lazima kwa wale wote wenye kutofautiana na kuzozana warudi katika misingi hii miwili: Qur-aan na Sunnah. Si halali kwa yeyote kupingana na maneno ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa maneno ya mtu yeyote vovyote atavyokuwa. Ikikubainikia haki basi ni lazima kuyapiga ukutani maneno ya anayekwenda kinyume na viwili hivyo na wala usimzingatie pasi na kujali kiwango alichonacho cha elimu na dini. Mtu anakosea lakini maneno ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuna ndani yake makosa.

Nasikitishwa kusikia kwamba kuna watu ambao wanazingatia watu ambao ni wakweli katika kuitafuta na kuifikia haki, lakini licha ya hivo tunawaona kuwa ni wenye kufarikiana. Kila mmoja katika wao ana jina na wasifu maalum. Hili ni kosa. Dini ya Allaah ni moja. Ummah wa Uislamu ni mmoja. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَإِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاتَّقُونِ

”Hakika huu ummah wenu ni ummah mmoja Nami ni Mola wenu. Hivyo nicheni.”[1]

Allaah (Subhaanah) amesema kumwambia Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا لَّسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ ۚ إِنَّمَا أَمْرُهُمْ إِلَى اللَّـهِ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ

“Hakika wale waliofarikisha dini yao na wakawa makundi makundi huna lolote kuhusiana na wao. Hakika amri yao iko kwa Allaah, kisha atawajulisha kwa yale waliyokuwa wakifanya.”[2]

شَرَعَ لَكُم مِّنَ الدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَىٰ ۖ أَنْ أَقِيمُوا الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ ۚ كَبُرَ عَلَى الْمُشْرِكِينَ مَا تَدْعُوهُمْ إِلَيْهِ ۚ اللَّـهُ يَجْتَبِي إِلَيْهِ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي إِلَيْهِ مَن يُنِيبُ

“Amekuwekeeni Shari´ah katika dini yale aliyomuusia kwayo Nuuh na ambayo tumekufunulia Wahy na tuliyomuusia kwayo Ibraahiym na Muusa na ‘Iysaa kwamba simamisheni dini na wala msifarikiane humo. Yamekuwa makubwa kwa washirikina yale unayowalingania. Allaah anamteua Kwake amtakaye na anamwongoza Kwake anayerudiarudia .”[3]

Ikiwa haya ndio maelekezo ya Allaah kwetu sisi, basi kilicho cha lazima kwetu sisi ni kuyashika maelekezo haya na tukusanyike kwenye meza ya majadiliano na tuhojiane sisi kwa sisi kwa njia ya matengenezo na si kwa njia ya ukosoaji wala kulipiza kisasi. Mtu yeyote ambaye anamjadili na kumuhoji mwingine kwa kukusudia maoni yake ndio yashinde na ayatweze maoni ya wengine au aidha kwa lengo la kukosoa pasi na kutengeneza, basi mara nyingi anatoka hali ya kuwa si mwenye kumridhisha Allaah na Mtume Wake.

Kwa hivyo ni wajibu katika mfano wa mambo haya tuwe Ummah mmoja. Simaanishi kwamba hakuna yeyote mwenye kukosea. Kila mmoja mara hukosea na mara hupatia. Lakini tunachozungumzia ni namna gani linarekebishwa kosa hili. Si njia ya sawa nikamzungumza nyuma ya mgongo na kumponda wakati ninaporekebisha kosa lake. Njia ya sawa ya kulirekebisha ni kukutana naye na kumuhoji. Baada ya hapo ikibainika kwamba mtu huyu anaendelea kuwa mkaidi na ile batili aliyomo, basi hapo mimi nina udhuru na haki. Bali nalazimika kubainisha kosa lake na kuwatahadharisha watu kutokamana na kosa lake. Mambo yanatengemaa namna hii. Ama mfarakano na kuwa makundimakundi ni jambo ambalo halimfurahishi yeyote. Isipokuwa ambaye ni adui wa Uislamu na waislamu.

Namuomba Allaah azikusanye nyoyo zetu katika kumtii, atujaalie kuwa miongoni mwa wenye kuhukumiana kwa Allaah na Mtume Wake, azitakase nia zetu na atubainishie yale yaliyofichikana kwetu katika Shari´ah Yake. Kwani hakika Yeye ni Mwingi wa kutoa, Mkarimu.

Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

[1] 23:52

[2] 06:159

[3] 23:53

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Zaad Daa´iyah ila Allaah, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 08/11/2021