16. Zawadi ya tano: Kuvunja vizuizi kati yako na watu

Mlinganizi anatakiwa kuvunja vizuizi vilivoko kati yake yeye na watu. Kwa sababu wengi katika ndugu zetu walinganizi wanapowaona watu wako wanafanya maasi basi ile ghera na kuyachukia yale maovu kunaweza kumpelekea kutowaendea watu hawa na wala asiwanasihi, jambo ambalo ni kosa na si hekima kabisa. Bali hekima ni yeye kwenda kulingania, akhofishe, awatie shauku na woga. Asionelee kuwa watu hao ni watenda madhambi ambao hawezi kutembea kando nao. Ikiwa wewe mlinganizi wa kiislamu huwezi kutembea karibu na watu hawa na wala kuwaendea kuwalingania katika dini ya Allaah, basi ni nani ambaye atawasaidia? Watawasaidia watu mfano wao? Watawasaidia watu wasiotambua? Kamwe. Kwa ajili hiyo mlinganizi anapaswa kusubiri. Hii ambayo tumetaja punde pia ni katika subira. Aisubirishe nafsi yake, achukie na avunje vikwazo kati yake yeye na watu ili aweze kuwafikishia ulinganizi wake wale ambao wanauhitajia. Ama kujizuilia, hilo ni kinyume na vile ambavo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivokuwa akifanya.

Kama inavotambulika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika masiku ya Minaa alikuwa akiwaendea washirikina maeneo yao na akiwalingania katika dini ya Allaah. Imepokelewa kutoka kwake kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Je, hakuna yeyote atakayenibeba ili niweze kuyafikisha maneno ya Mola wangu? Kwani hakika Quraysh wamenizuia kuyafikisha maneno ya Mola wangu.”[1]

Ikiwa huu ndio mwenendo wa Mtume, kiongozi na kiigizo chetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi ni katika wajibu kwetu sisi tuwe mfano wake inapokuja katika suala la kulingania katika dini ya Allaah.

[1] Ahmad (14510), (14511) na (14708) na Ibn Hibbaan (6274).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Zaad Daa´iyah ila Allaah, uk. 21-22
  • Imechapishwa: 08/11/2021