17. Wasichana kuchelewesha kuolewa kwa sababu ya masomo na kazi

Swali 17: Kuna ada iliyoenea ambayo ni msichana kukataa kuolewa au baba yake kumkatalia yule mposaji ili akamilishe masomo yake ya sekondari, chuo kikuu au masomo kwa muda wa miaka kadhaa. Ni ipi hukumu ya hilo na ni zipi nasaha zako kwa wenye kufanya hivo? Wakati mwingine wanawake wanaenda mpaka miaka thelathini au zaidi na bado hawajaolewa.

Jibu: Hukumu ya hilo ni kwenda kinyume na amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atapokujieni yule ambaye mmeiridhia dini na tabia yake basi muozesheni.”

“Enyi kongamano la vijana! Yule miongoni mwenu mwenye uwezo wa kuoa na afanye hivyo, kwani hilo linamfanya ainamishe macho yake na inahifadhi utupu wake.”

Kujizuilia na ndoa kunapelekea kukosa manufaa mengi ya ndoa. Kwa ajili hiyo nawanasihi ndugu zangu waislamu ambao ndio wasimamizi wa wanawake na pia dada zangu wa kiislamu, wasikatae kuolewa kwa sababu ya kukamilisha masomo. Wanachoweza kufanya ni mwanamke kumuwekea sharti mwanamme kuendelea na masomo yake mpaka atakapomaliza, au kuendelea na kazi yake ya kufundisha kwa kipindi cha mwaka mmoja au miaka miwili, muda wa kuwa hakushughulishwa kutokamana na watoto wake. Mwanamke kuzama katika elimu ya vyuo vikuu, ambazo hatuzihitaji, ni jambo linatakiwa kuangaliwa vyema. Kile ninachoona ni kuwa inatosha kwa mwanamke kumaliza masomo yake ya hatua ya awali na akawa anajua kusoma na kuandika kwa njia ya kwamba atanufaika kwa elimu yake hii kuweza kusoma Kitabu cha Allaah, tafsiri yake na kusoma Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maelezo yake. Labda azame kusoma elimu ambazo watu wanazihitaji kama mfano wa elimu ya udaktari na mfano wake muda wa kuwa katika kusoma kwake hakuna mambo yanayokataliwa na Shari´ah kama vile kuchanganyika kwa wanamme na wanawake na mambo mfano wake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 01/03/2023