16. Ni ipi hukumu ya kukata nywele za wasichana kufika mabegani kwa ajili ya kujipamba, ni mamoja anyefanya hivo ameolewa au hakuolewa?

Swali 16: Ni ipi hukumu ya kukata nywele za wasichana kufika mabegani kwa ajili ya kujipamba, ni mamoja anyefanya hivo ameolewa au hakuolewa? Ni ipi hukumu ya kuvaa viatu vyenye visigino virefu, ni mamoja virefu sana au kidogo? Ni ipi hukumu ya kutumia zana za vipodozi vinavyotambulika kwa ajili ya kumpambia mume?

Jibu: Ni haramu kwa mwanamke kukata nywele zake kwa njia ya kufanana na nywele za wanamme na inahesabika ni miongoni mwa madhambi makubwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanawake wenye kujifananisha na wanamme. Hali nyingine ni kukata nywele kwa njia isiyokuwa na kufanana na wanamme, wanazuoni wametofautiana katika maoni matatu:

1 – Wako waliosema kuwa inafaa na hapana vibaya.

2 – Wengine wakasema kuwa ni haramu.

3 – Baadhi ya wengine wakasema kuwa inachukiza.

Kinachotambulika katika madhehebu ya Imaam Ahmad ni kwamba inachukiza. Ukweli wa mambo – kama tulivyotangulia kutaja katika jibu lililotangulia – ni kwamba haitakiwi kwetu kupokea kila desturi zisizokuwa zetu. Sisi muda si mrefu sana tulikuwa tunawaona wanawake wanajisifu ni nani kati yao mwenye nywele nyingi zaidi kichwani au mwenye nywele refu zaidi. Ni kwa nini basi wanayaendea matendo yaliyotoka nje ya nchi isiyokuwa yetu? Mimi sipingi kila kipya, lakini mimi napinga kila kitu ambacho kinapelekea jamii kwenda katika ada zinazotoka kwa wasiokuwa waislamu.

Kuhusu viatu vyenye kisigino kirefu havijuzu vinavyopingana na desturi na pia kupelekea kuonyesha mapambo na kuwafanya wanamme kumwelekezea macho. Allaah amesema:

وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَى

“Tulizaneni majumbani mwenu na wala msijishauwe kwa kuonyesha mapambo kama walivyojishauwa zama za ujahili.”[1]

Kila kitu ambacho maana yake ni kuonyesha mapambo na kudhihiri kwake na akajitofautisha na wanawake wengine kwa njia ya kujipamba, ni haramu na hakijuzu.

Kuhusu kutumia zana za vipodozi, kama kuifanya midomo kuwa miekundu na kuyafanya mashavu kuwa mekundu, haina neno na khaswa ikiwa ni mwanamke aliyeolewa. Kuhusu mapambo yanayofanywa na baadhi ya wanawake ambapo wanaondosha na kuchonga nyusi ni haramu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanawake wenye kuchonga na wenye kuchongwa nyusi na pia mwanamke mwenye kuyapamba meno yake ili yaonekane mazuri.

[1] 33:33

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah, uk. 25-26
  • Imechapishwa: 01/03/2023