Abu Mansuur bin Hamshaad ametuhadithia: Abu ´Aliy Ismaa´iyl bin Muhammad as-Saffaar ametuhadithia Baghdad: Abu Mansuur ar-Ramaadiy ametuhadithia: ´Abdur-Razzaaq ametuhadithia: Ma´mar ametukhabarisha, kutoka kwa Suhayl bin Abiy Swaalih, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Abu Hurayrah, aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah (Ta´ala) anashuka katika kila usiku katika mbingu ya dunia na akasema mpaka kupambazuke: ”Mimi ni Mfalme! Mimi ni Mfalme! Nani mwenye kuniomba Nimuitikie? Nani mwenye kuniomba du´aa Nimjibie? Nani mwenye kuniomba msamaha Nimsamehe?”

Baada ya Mansuur kutusomea Hadiyth hii, nilimsikia akisema:

”Abu Haniyfah aliulizwa juu yake ambapo akajibu: ”Anashuka chini, bila kufanyiwa namna.” Wengine wamesema: ”Anashuka chini ushukaji ambao unalingana na uola Wake. Halitakiwi kufanyiwa namna na pasi na ushukaji Wake kulinganishwa na ushukaji wa viumbe kwa njia ya kuhama na kushughulishwa. Kwa sababu Yeye (Jalla wa ´Alaa) ametakasika sifa Zake kufanana na sifa za viumbe, kama ambavo dhati Yake imetakasika kufanana na dhati za viumbe. Kuja, ujio na kushuka Kwake ni kwa njia inayolingana na sifa Zake, bila kufananisha wala kuzifanyia namna.”

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 220-223
  • Imechapishwa: 10/12/2023