17. Qur-aan ni maneno ya Allaah na haikuumbwa

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Qur-aan ni maneno ya Allaah na hayakuumbwa. Mtu asidhoofike kusema kuwa hayakuumbwa. Hakika maneno ya Allaah hayakutengana Naye na hakuna kitu katika Yeye ambacho kimeumbwa. Ninakuonya kujadiliana na wale waliozusha katika jambo hili. Mwenye kusema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumbwa au akasimama na kusema:

“Sijui kama imeumbwa au haikuumbwa – si jengine Qur-aan ni maneno ya Allaah.”

ni jitu la Bid´ah ni kama yule mwenye kusema kuwa imeumbwa. Qur-aan ni maneno ya Allaah na haikuumbwa.”

MAELEZO

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema kuwa Qur-aan ni maneno Yake:

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ

“Ikiwa mmoja wa washirikina akikuomba umlinde, basi mlinde mpaka ayasikie maneno ya Allaah.”[1]

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ

”Tanabahi! Uumbaji ni Wake pekee na kupitisha amri.”[2]

 Ibn ´Uyaynah na wengineo wamesema:

“Viumbe ni viumbe vya Allaah na amri ni Qur-aan.”[3]

´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Qur-aan  ni maneno ya Allaah. Hivyo basi msikinzane nayo kwa maoni yenu.”[4]

Maalik amesema:

“Qur-aan ni maneno ya Allaah.”

Alionekana ni mwenye kuchukizwa na yule mwenye kusema kwamba Qur-aan imeumbwa. Maalik amesema:

“Anatakiwa kuchapwa bakora na kutiwa jela mpaka afe.”

ash-Shaafi´iy amesema:

“Qur-aan ni maneno ya Allaah na haikuumbwa. Mwenye kusema kuwa imeumbwa ni kafiri.”[5]

Imaam Ahmad alifungwa gerezani na akateswa mpaka akapoteza fahamu. Alikuwa akitenzwa nguvu kusema kwamba Qur-aan imeumbwa, lakini akikataa na kuwauliza ni vipi atasema kitu kinachopingana na yale aliyosema Allaah (´Azza wa Jall) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivo ndivo Allaah alimfanya akaitia nguvu Sunnah na kuinusuru haki. Kupitia yeye ikabainika njia iliyonyooka baada ya kukurubia kuondoka. Yeye ndiye imamu wa Ahl-us-Sunnah kwa haki. Baadhi ya Salaf wamesema:

“Allaah aliunusuru Uislamu kwa Abu Bakr as-Swiddiyq wakati wa kuritadi na kwa Ahmad bin Hanbal wakati wa mtihani.”

Ni imamu wa aina gani aliyekuwa! Allaah amrehemu, wema na Salaf wote walioifuata haki na wanaopambana kwa ajili ya kuidhihirisha. Allaah atufufue pamoja nao licha ya kasoro tulizonazo.

[1] 09:06

[2] 07:54

[3] ash-Shariy´ah (77) ya al-Aajurriy.

[4] ash-Shariy´ah (156) ya al-Aajurriy.

[5] ash-Shariy´ah (166) ya al-Aajurriy.

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 98-101
  • Imechapishwa: 09/04/2019