16. Imechukizwa na kukatazwa kubishana juu ya Qadar, Kuonekana na Qur-aan

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Lililo juu yake ni kuziamini na asirudishe herufi hata moja kwenye Hadiyth hizo au nyenginezo zilizopokelewa kutoka kwa wapokezi waaminifu. Asivutane wala kubishana na yeyote. Wala asijifunze mijadala. Mizozano juu ya Qadar, Kuonekana, Qur-aan na mambo mengine ya I´tiqaad ni jambo limechukizwa na limekatazwa. Mwenye kufanya hivo sio katika Ahl-us-Sunnah – japokuwa atazungumza kwa ´Aqiydah – mpaka pale atapoacha mijadala na kujisalimisha na kuamini mapokezi.”

MAELEZO

Anachotakiwa ni yeye kuamini na asirudishe herufi hata moja kutoka kwenye Hadiyth zinazozungumzia Qadar na mfano wake.

Imekatazwa kubishana juu ya Qadar, kwa sababu Qadar ni siri ya Allaah isiyojua yeyote. Hakuna yeyote anayejua yaliyomo ndani yake isipokuwa Allaah. Haifai kwetu kukosoa, kukinzana wala kujadili katika mambo haya. Kwa sababu mijadala katika maudhui haya haipelekei natija yoyote. Bali huenda mijadala kama hiyo ikampelekea mja kuingiwa na mashaka. Ni wajibu kwako mja kutambua kwamba unatakiwa kujiepusha na mijadala na ubishi kuhusu Qadar. Hayo ni kutokana na manufaa yako mwenyewe. Ukisikia utata unaotajwa na mzushi kuna khatari kukaingia na kukita kitu moyoni mwako na matokeo yake ukaanza kuwa na mashaka baada ya kuwa ni mwenye yakini na muumini. Mche Allaah juu ya nafsi yako! Jaribu kujiepusha na mambo haya. Mwenye kuingia ndani ya mambo haya anaangamia. Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwasikia Maswahabah wakibishana juu ya Qur-aan. Akakasirika sana kiasi cha kwamba uso wake ukawa kama mbegu ya komamanga na akasema:

“Je, haya ndio mmeamrishwa?”[1]

[1] Ibn Maajah (85).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 96-97
  • Imechapishwa: 09/04/2019