17. Mfumo wa ulinganizi ni lazima uwe kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah

Swali 17: Mfumo wa kulingania kwa Allaah unatakiwa uwe kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah au inafaa kwa kila mmoja kulingania vile anavyoona yeye?

Jibu: Mfumo wa ulinganizi unapaswa uwe kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah. Qur-aan, Sunnah na historia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[1] umeyabainisha. Tusizue kitu kutoka kwetu wenyewe. Namna ya kulingania kumetajwa katika Qur-aan na Sunnah. Tukianza kuzua tutapotea sisi na kupotosha wengine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”[2]

Hata hivyo ni kweli ya kwamba leo tunatumia njia ambazo hazikuwepo hapo kabla, ikiwa ni pamoja na vipaza sauti, redio, majarida, magazeti, marusho ya moja kwa moja na TV. Hizi ni njia ambazo ulinganizi unanufaika kwazo. Hata hivyo sio mfumo. Mfumo Allaah (Ta´ala) ameubainisha pale aliposema:

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.”[3]

Vivyo hivyo mfumo wa ulinganizi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alipokuwa Makkah na Madiynah:

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

“Hakika mna kigezo kizuri kwa Mtume wa Allaah kwa mwenye kumtaraji Allaah na Siku ya Mwisho na akamtaja Allaah kwa wingi.”[4]

[1] Allaah (Ta´ala) ametukamilishia dini. Kwa hivyo hakuna mtu yeyote yuko na haki ya kuzua njia yake kulingania katika Uislamu. Mwenye kufanya hivo atakuwa anasema, japo si moja kwa moja, ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakufikisha ujumbe kikamilifu na kwamba mifumo mingine inanufaisha na kuathiri zaidi.

Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomtuma Mu´aadh bin Jibal (Radhiya Allaahu ´anh) kwenda Yemen alimwambia:

“Hakika unawaendea watu katika Ahl-ul-Kitaab. Kitu cha kwanza kuwalingania iwe ni hapana mungu mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Katika upokezi mwingine imekuja wamuabudu Allaah peke yake. Wakikutii katika hilo, wafunze kuwa Allaah amewafaradhishia swalah tano kwa siku. Wakikutii katika hilo, wafunze kuwa Allaah amewawajibishia zakaah ambayo itachukuliwa kutoka kwa matajiri wao na kupewa mafakiri wao. Wakikutii katika hilo, jiepushe na dhuluma. Tahadhari na du´aa ya mdhulumiwaji; hakika hakuna kati ya du´aa hiyo na Allaah kizuizi.” (al-Bukhaariy (1331))

Hii ni dalili ya wazi kabisa yenye kuonyesha kuwa mfumo wa ulinganizi unapaswa kuwa kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah. Vinginevyo Mu´aadh bin Jabal alikuwa ni mwenye kustahiki zaidi kwa ulinganizi kuliko walinganizi elfu moja hii leo. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah aliulizwa juu ya mtu anayewalingania watu katika Uislamu na tawbah kwa njia ya nyimbo. Chini kunakuja swali na jawabu:

“Kikosi cha watu kinakusanyika juu ya madhambi makubwa, ikiwa ni pamoja na kuua, kupora, kuiba, kunywa pombe na mengineyo. Shaykh mmoja ambaye anatambulika kwa kheri na kufuata Sunnah akakusudia kuwakataza watu hao kutokamana na mambo hayo na hakuweza kuwafikia kwa njia nyingine isipokuwa kwa nyimbo na kwa nia hii. Kulipigwa matari na kukaimbwa mashairi yanayoruhusiwa pasi na vipengele vyovyote vya ujana. Baada ya yeye kufanya hivo vijana wengi walitubia. Matokeo yake akawa yule ambaye haswali wala hatoi zakaah na pia anaiba sasa anajiepusha na mambo yenye utata, anatekeleza mambo ya faradhi na anajiepusha na mmbo ya haramu. Je, inaruhusiwa kwa Shaykh huyu kuimba kwa njia hii kutokana na yale manufaa yanayopelekea katika jambo hilo na kwamba hawezi kuwalingania kwa njia nyingine isipokuwa hii tu?”

Akajibu (Rahimahu Allaah):

“Himdi zote anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu.

Msingi wa kujibu swali hili na mengine mfano wake, mtu anatambua kuwa Allaah amemtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa uongofu na dini ya haki ili izishinde dini zingine zote. Aidha itambulike kuwa Allaah amemkamilishia yeye na Ummah wake dini. Amesema (Ta´ala):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

”Leo Nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.”[1]

Yule mwenye kumtii amebashiriwa furaha, na yule mwenye kumuasi amebashiriwa kula khasara. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يُطِعِ اللّهَ وَالرَّسُولَ فَأُوْلَئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللّهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاء وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَئِكَ رَفِيقًا

“Atakayemtii Allaah na Mtume basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah aliowaneemesha – Manabii na wakweli na mashahidi na waja wema – na uzuri ulioje kuwa na tangamano kama hili!”[1]

وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا

“Yeyote atakayemuasi Allaah na Mtume Wake, basi hakika atapata Moto wa Jahannam hali ya kudumu humo milele.”[1]

Amewaamrisha viumbe wakati wa kukhitilafiana kuhusu mambo ya dini basi warudishe katika yale aliyomtumiliza nayo. Amesema (Ta´ala):

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

”Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[1]

Allaah ameeleza kuwa yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) analingania kwa Allaah na katika njia Yake ilionyooka:

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi – mimi na anayenifuata.”[1]

وَلَـٰكِن جَعَلْنَاهُ نُورًا نَّهْدِي بِهِ مَن نَّشَاءُ مِنْ عِبَادِنَا ۚ وَإِنَّكَ لَتَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ صِرَاطِ اللَّـهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ أَلَا إِلَى اللَّـهِ تَصِيرُ الْأُمُورُ

”… lakini tumeijaalia kuwa ni nuru, tunamwongoza kwayo Tumtakaye kati ya waja Wetu. Na hakika wewe bila shaka unaongoza kuelekea njia iliyonyooka – Njia ya Allaah ambaye ni Vyake pekee vyote vilivyomo mbinguni na vyote vilivyomo ardhini. Tanabahi! [Kuwa ni] kwa Allaah pekee yanaishia mambo yote.”[1]

Ameeleza kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaamrisha mema, anakataza maovu, anahalalisha vilivyo vizuri na anaharamisha vilivyo vibaya:

وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ ۚ فَسَأَكْتُبُهَا لِلَّذِينَ يَتَّقُونَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَالَّذِينَ هُم بِآيَاتِنَا يُؤْمِنُونَ الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالْأَغْلَالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ ۚ فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ ۙ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

”Rehema Yangu imekienea kila kitu. Basi nitawahukumia wale wenye kumcha Allaah na wanaotoa zakaah na ambao wao wanaziamini Aayah Zetu. Wale wanomfuata Mtume, Nabii asiyejua kuandika na kusoma, wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawraat na Injiyl anawaamrisha mema na anawakataza maovu na anawahalalishia vizuri na anawaharamishia vibaya na anawaondoshea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao. Basi wale waliomwamini na wakamtukuza na wakamnusuru na wakafata Nuru ambayo imeteremshwa pamoja naye – hao ndio wenye kufaulu.”[1]

Allaah amemwamrisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mema yote, akamkataza maovu yote, akahalalisha kila kilicho kizuri na akaharamisha kila kilicho kibaya. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah hajapatapo kumtuma Mtume yeyote isipokuwa ilikuwa ni haki juu yake kuuelekeza Ummah wake katika kheri anayoifahamu juu yao na kuwaonya na shari anayoifahamu juu yao.”[1]

 al-´Irbaadhw bin Saariyah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituwaidhi mawaidha ambayo nyoyo ziliingiwa na khofu kwayo na macho yakatokwa na machozi. Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni kana kwamba ni mawaidha ya kutuaga, hivyo basi tuusie.” Akasema: “Nimekuacheni juu ya weupe ambao usiku wake ni kama mchana wake; hatopotea nayo isipokuwa mstahiki maangamivu. Hakika yule atakayeishi muda mrefu katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza. Ziumeni kwa magego yenu. Na nakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah.”[1]

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Eyi watu! Hakuna chochote kinachokuwekeni karibu na Pepo na kukuweni mbali na Moto isipokuwa nimekuamrisheni nacho, na hakuna chochote kinachokuwekeni mbali na Pepo na kukusogezeni karibu na Moto isipokuwa nimekukatazeni nacho.”[1]

 al-´Irbaadhw bin Saariyahamesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimekuacheni katika weupe; usiku wake ni kama mchana wake. Hakuna anayepotea humo isipokuwa anayestahiki kuangamia.”[1]

Kanuni hii tukufu na yenye kuenea imetajwa katika Qur-aan na Sunnah. Wanazuoni, akiwemo al-Bukhaariy na al-Baghawiy, wameiwekeakichwa cha khabari. Kwa hivyo yule anayeshikamana na Qur-aan na Sunnah basi ni katika mawalii wa Allaah na wenye kumcha, kundi lake lililofaulu na jeshi Lake lililoshinda. Salaf walikuwa wakisema:

“Sunnah ni kama safina ya Nuuh; yule mwenye kuipanda anaokoka na yule mwenye kubaki nyuma anazama.”

az-Zuhriy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Wanazuoni wetu waliotangulia walikuwa wakisema: “Kushikamana na Sunnah ni kuokoka.”[1]

Yakishatambulika haya basi ni lazima yale ambayo Allaah anawaongoza kwayo wapotofu, anawaelekeza waliopotoka na anawasamehe watenda madhambi yawe katika ule ujumbe ambao amemtumiliza kwao Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Qur-aan na Sunnah. Vinginevyo endapo ule ujumbe ambao Allaah amemtumiliza kwao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hautoshi kwa jambo hilo, basi dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ingelikuwa pungufu na yenye kuhitaji kukamilishwa.

Jengine mtu anatakiwa kujua kuwa matendo mema ambayo Allaah ameamrisha ima iwe kwa njia ya ulazima au kwa njia ya mapendekezo. Allaah amekataza pia matendo mabovu. Kama kitendo kimekusanya manufaa na madhara, hekima ya Mwekaji Shari´ah ni kwamba ikiwa manufaa yake yatashinda madhara yake, anakiweka kitu hicho katika Shari´ah, na ikiwa madhara yake yanashinda manufaa yake, hakiweki katika Shari´ah – kinyume chake anakikataza. Allaah (Ta´ala) amesema:

كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ وَهُوَ كُرْهٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

”Mmeandikiwa kupigana vita nako ni chukizo kwenu na huenda mkachukia jambo na hali lenyewe ni kheri kwenu na huenda mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu; na Allaah anajua na nyinyi hamjui.”[1]

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ ۖ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا

”Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: “Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na manufaa [fulani] kwa watu; na dhambi yake viwili hivyo ni kubwa kuliko manufaa yake.”[1]

Kwa ajili hiyo ndio maana Allaah (Ta´ala) akayaharamisha baada ya hapo.

Vivyo hivyo yale matendo ambayo watu wanaona kuwa yanawakurubisha mbele ya Allaahlakini Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)hawakuyaweka katika Shari´ah; ni lazima madhara yake yawe makubwa zaidi kuliko manufaa yake. Kwa sababu manufaa yake yangelikuwa makubwa zaidi kuliko madhara yake, basi Shari´ah isingeyapuuza. Yeye ni Mwingi wa hekima na hapuuzi manufaa ya dini na wala yale mambo ambayo yanawafanya waumini kuwa karibu na Mola wa walimwengu.

Shaykh aliyetajwa kushindwa kuwafanya watenda madhambi makubwa wakatubia isipokuwa kwa njia ya mfumo uliyozuliwa ambao umetajwa katika swali, ni dalili inayofahamisha kuwa Shaykh huyo ni mjinga wa mifumo iliyowekwa katika Shari´ah ambayo kwayo wanasamehewa watenda madhambi makubwa au mifumo hiyo imemshinda. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah na wanafunzi wa Maswahabah walikuwa wakiwalingania walio waovu zaidi kuliko watu hawa – katika makafiri, watenda madhambi na maasi – na walifanya hivo kwa kutumia zile njia zilizowekwa katika Shari´ah. Allaah aliwatosheleza nazo kutokamana na mifumo iliyozuliwa. Haijuzu kusema kuwa Allaah hakumtuma Mtume Wake kwa mifumo iliyowekwa katika Shari´ah ambayo inaweza kuwafanya watenda madhambi wakatubia. Ni jambo linalotambulika vyema na kwa mapokezi mengi kwamba Allaah (Ta´ala) aliwasamehe makafiri wengi wasiohesabika kutokamana na ukafiri, ufuska na maasi kutokana na ile mifumo iliyowekwa katika Shari´ah ambayo haina hiyo mikusanyiko ya Bid´ahiliyotajwa. Bali wale wa awali waliotangulia, wale wahamaji na wanusuraji, na wale waliowafuata kwa wema, walitubu kwa Allaah (Ta´ala) kwa mifumo iliyowekwa katika Shari´ah na si kwa mifumo hii iliyozuliwa. Miji na vijiji vya waislamukatika nyakati zote imejaa watu waliotubu kwa Allaah na wakamcha Allaah na wakafanya yale mambo yanayopendwa na Allaah na kumfurahisha kwa kutumia njia zilizowekwa katika Shari´ah na si kwa njia hizi za Bid´ah.

Kwa hivyo haiwezekani kusema kwamba watenda maasi hawawezi kutubia isipokuwa kwa njia hizi za kizushi. Bali mtu anaweza kusema kuwa kuna Mashaykh ambao ni wajinga juu ya taratibu hizi zilizowekwa katika Shari´ah na zenye kuwashinda, hawana elimu ya Qur-aan na Sunnah na yale anayotakiwa kuwazungumzisha watu na kuwasikilizisha nayo katika yale ambayo Allaah hufanya akawasamehe kwayo, ambapo Shaykh huyu akapondoka kutokamana na njia zilizowekwa katika Shari´ah na badala yake akaziendea zile zilizozuliwa. Ima akafanya hivo kutokamana na nia njema – akiwa ni mtu wa dini – au ikawa lengo lake ni kutaka kuwa na utawala juu yao na kula mali zao kwa batili.” (Majmuu´-ul-Fataawaa (11/620-624))

Zingatia mifumo hii iliyozushwa na ilinganishe na yale ambayo walinganizi na mapote ya leo wanaita “mifumo ya ulinganizi”; kucheza mpira, Anaashiyd wanazoita kuwa ni za Kiislamu, michezo ya kuigiza wanayoita kuwa ni ya Kiislamu, safari za huku na huku na visa.

[2] al-Bukhaariy (3550) na Muslim (1718).

[3] 16:125

[4] 33:21

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 43-45
  • Imechapishwa: 31/05/2023
  • mkusanyaji: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy