Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Mfano wa aina za ´ibaadah ambazo Allaah Ameamrisha ni Uislamu, Imani na Ihsaan. Miongoni mwa hizo ni Du´aa pia, khofu, matarajio, utegemeaji, shauku [raghbah] na woga [rahbah], unyenyekeaji, tisho, kurejea [inaabah], kutaka msaada, kutaka kinga, kutaka kuokolewa, kuchinja, kuweka nadhiri na aina nyinginezo zote miongoni mwa aina za ´ibaadah ambazo Allaah Ameamrisha. Zote ziwe kwa
ajili ya Allaah Pekee. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Sehemu zote za kuswalia ni kwa ajili ya Allaah, basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.” (72:18)

Mwenye kumtekelezea chochote katika hayo mwengine asiyekuwa Allaah ni mshirikina kafiri. Dalili ya hilo ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚإِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine hana ushahidi wowote juu ya hilo, basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake, kwani hakika hawafaulu makafiri.” (al-Mu´minuun 23:117)

Katika Hadiyth imekuja:

“Du´aa ndio kiini cha ´ibaadah.”

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ

“Mola wenu Amesema: “Niombeni, Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari na ‘Ibaadah Yangu, watauingika Motoni.” (Ghaafir 40 : 60)

MAELEZO

Kuna sampuli mbalimbali za ´ibaadah. Moja wapo ni Uislamu na nguzo zake. Matendo yote ya Kiislamu, kama swalah na swawm, alivyoamrisha Allaah ni ´ibaadah. Vivyo hivyo inahusiana na imani na matendo yake ya ndani kama kumuamini Allaah, Malaika, Vitabu Vyake, Mitume Wake, siku ya Qiyaamah na Qadar kheri na shari yake. Khofu, mapenzi na matarajio ni mfano wa ´ibaadah. Yote yanayohusiana na moyo ni ´ibaadah. Kadhalika Ihsaan ambayo ni kumuabudu Allaah kama vile unamuona. Ni katika ´ibaadah, bali ndio iliyo juu na aina kubwa ya ´ibaadah.

Lililo la wajibu kwa kila muislamu ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia amtakasie ´ibaadah Allaah pekee. Asiombe pamoja na Allaah Mitume, mawalii, masanamu, miti, mawe wala nyota. ´Ibaadah ni haki ya Allaah pekee. Amesema (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Sehemu zote za kuswalia ni kwa ajili ya Allaah, basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.” (72:18)

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

“Wewe pekee ndiye tunakuabudu na Wewe pekee ndiye tunakuomba msaada.” (01:05)

وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ

“Wala yeyote usiombe badala ya Allaah asiyekufaa na wala asiyekudhuru. Ukifanya hivyo, basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.” (10:106)

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚإِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine hana ushahidi wowote juu ya hilo, basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake, kwani hakika hawafaulu makafiri.” (23:117)

يُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَيُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ ۚ وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ۚ وَلَا يُنَبِّئُكَ مِثْلُ خَبِيرٍ

“Anauingiza usiku katika mchana na anauingiza mchana katika usiku na anaitisha jua na mwezi: kila kimoja kinakwenda mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Huyo ndiye Allaah, Mola wenu! Ufalme ni Wake pekee, na wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki [chochote hata] kijiwavu cha kokwa ya tende! Mkiwaomba hawasikii maombi yenu, na hata wakisikia hawatakuitikieni. Na siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu. Na wala hakuna yeyote atakayekujulisha [haki] kama Yeye mkhabarishaji.” (35:13-14)

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 08/12/2016