97. Inapobaki roho baada ya kutoka kwenye kiwiliwili

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ ۖ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي

“Wanakuuliza kuhusu roho. Sema: “Roho ni katika amri ya Mola wangu.” 17:85

فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ

“Nitakapomsawazisha na nikampuliza kitu katika roho Yangu, basi muangukieni kumsujudia.” 15:29

وَمَرْيَمَ ابْنَتَ عِمْرَانَ الَّتِي أَحْصَنَتْ فَرْجَهَا فَنَفَخْنَا فِيهِ مِن رُّوحِنَا

“[Mfano mwingine tena wako nao kwa] Maryam, binti wa ‘Imraan; ambaye amehifadhi ubikira wake Tukampulizia humo kutoka roho Yetu.” 66:12

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Halafu hutumiwa Malaika akampulizia roho.”

Kuhusu maneno ya Allaah (Ta´ala):

فَأَرْسَلْنَا إِلَيْهَا رُوحَنَا فَتَمَثَّلَ لَهَا بَشَرًا سَوِيًّا

“Tukamtumia roho Yetu akajimithilisha kwake kama [umbile] sawa na mtu.” 19:17

na:

يَوْمَ يَقُومُ الرُّوحُ وَالْمَلَائِكَةُ صَفًّاۖ لَّا يَتَكَلَّمُونَ إِلَّا مَنْ أَذِنَ لَهُ الرَّحْمَـٰنُ وَقَالَ صَوَابًا

“Siku atakayosimama roho na Malaika safu kwa safu [na hakuna] yeyote atakayezungumza isipokuwa yule ambaye Mwingi wa Rahmah amempa idhini na hatosema mengine isipokuwa yale yaliyo ya sawa na ya kweli.” 78:38

wafasiri wa Qur-aan wametofautiana kama inamlenga Jibriy au Malaika mwingine.

Wanachuoni wameandika sana juu ya mada hii, lakini sio kwa mpangilio kama huu. Nitataja maneno mafupi, lakini kwa njia yenye kuenea, ya wanachuoni wengi juu ya kubaki kwa roho ya mtu baada ya kufa kwake mpaka pale Qiyaamah kinaposimama. Je, roho inakuwa mbinguni au ardhini? Je, inakuwa Peponi au Motoni? Inahisi kuneemeka au kuadhibiwa kwenye viwiliwili vyake vya zamani au huhamishwa kwenye viwiliwili vingine visivyokuwa viwiliviwili vyao vya zamani? Huachwa huru au hutokomea kikamilifu? Wanachuoni wametaja maoni na kutofautiana kiasi kikubwa juu ya suala hilo. Kila kundi lina maoni yake linayoyasapoti na kuonelea kuwa ndio yenye nguvu kuliko ya wengine.

Suala hili linaweza kutambulika tu kupitia Wahy. Kuna wanachuoni waliosema kuwa roho za waumini na mashahidi ziko Peponi kwa sharti zisiwe zimefanya dhambi kubwa, kama kuwadhulumu waja, katika hali hiyo zitazuiwa na hilo. Ikiwa zimesalimika na mfano wa hayo basi zitakutana na Mola wao kwa msamaha na huruma:

وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتًا ۚ بَلْ أَحْيَاءٌ عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ

“Na wala usiwadhanie wale waliouawa katika njia ya Allaah wamekufa. Bali wahai kwa Mola wao wanaruzukiwa.” 03:169

Haya ndio maoni ikiwa ni pamoja vilevile na Abu Hurayrah, ´Abdullaah bin ´Umar na wengine katika Salaf. ´Abdullaah bin Ahmad ameeleza kuwa Imaam Ahmad amesema:

“Roho za waumini ziko Peponi na roho za makafiri ziko Motoni.”

Wengine wakasema roho za waumini ziko kwenye milango ya Peponi zikipata rehema, neema na riziki zake.

Abu ´Abdillaah bin Mandah amesema:

“Kundi la wanachuoni katika Maswahabah na Taabi´uun wamesema kuwa roho za waumini ziko kwa Allaah (´Azza wa Jall) bila ya kuzidisha neno juu ya hilo.”

Kisha akasema:

“Imepokelewa kutoka kwa Maswahabah na Taabi´uun wengi ya kwamba roho za waumini ziko Jaabiyah na roho za makafiri ziko kwenye kisima cha Barhuut Hadhwramawt.”

Abu ´Umar bin ´Abdil-Barr amesema:

“Roho za mashahidi ziko Peponi. Roho za waumini wengine ziko kwenye makaburi yao.”

Ibn-ul-Mubaarak amesimulia kuwa Ibn Shurayj alimsomea kwamba Mujaahid amesema:

“Roho za waumini ziko Peponi. Huko zinakula kwenye matunda yake na zinahisi harufu yake.”

Maalik amesema:

“Nimefikiwa na khabari kuwa roho iko huru. Inakwenda inapotaka.”

Ka´b-ul-Ahbaar amesema:

“Roho za waumini ziko ´Iliyyuun katika mbingu ya saba na roho za makafiri ziko katika Sijjiyn katika ardhi ya saba.”

Imepokelewa kwamba Abu Hurayrah amesema:

“Roho za wema ziko katika ´Iliyyuun na roho za watenda madhambi ziko katika Sijjiyn.”

Yamepokelewa mfano wa hayo kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Umar.

Kuna wanachuoni wanaosema kuwa roho za waumini ziko kwenye kisima cha Zamzam. Hata hivyo sijaona dalili ya maoni haya. Walio na maoni haya wanasema pia kuwa roho za makafiri ziko kwenye kisima cha Barhuut.

Salmaan al-Faarisiy amesema:

“Roho za waumini zinaenda zinakotaka na roho za makafiri ziko katika Sijjiyn.”

Ibn Qutaybah amesema:

“Wanachuoni wengi wanaonelea kuwa roho za waumini ziko kwenye makaburi yao. Kuna katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah waliosema kuwa roho za waumini na makafiri ziko ndani ya makaburi yao na kwamba zinaneemeshwa na kuadhibiwa ndani ya makaburi mpaka siku ya Qiyaamah, kama alivyoeleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na kwamba kaburi ima ni bustani miongoni mwa mabustani ya Peponi au ni shimo miongoni mwa mashimo ya Motoni. Ndio maana akawa amekataza kuyakalia na akaamrisha kuyatolea salamu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Pindi mmoja wenu anapokufa huonyeshwa mahala pake asubuhi na jioni. Akiwa ni katika watu wa Peponi, ni katika watu wa Peponi. Akiwa ni katika watu wa Motoni, ni katika watu wa Motoni. Ataambiwa: “Hapa ndipo mahala pako mpaka hapo Allaah atapokufufua siku ya Qiyaamah.”

Kuna wanachuoni wengine waliosema kuwa roho inabaki katika mbingu ya chini ya dunia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa katika safari yake ya mbinguni alimuona Aadam (´alayhis-Salaam) katika mbingu ya dunia na upande wake wa kulia kulikuwa roho za watu wenye furaha na upande wake wa kushoto kulikuwa roho za watu waliokula khasara. Katika haya ni yale aliyopokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Samurah bin Jundub aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu ndoto yake:

“Ama yule mwanaume mrefu ni Ibraahiym (´alayhis-Salaam) na wale watoto waliomzunguka wote ni watoto waliokufa katika maumbile.” Kukasemwa: “Ee Mtume wa Allaah! Mpaka watoto wa washirikina?” Akasema: “Hata watoto wa washirikina.”

Hata hivyo Hadiyth hii sio yenye kuenea. Inahusu tu roho za watoto wadogo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 210-212
  • Imechapishwa: 08/12/2016