Swali 17: Nimeona kwamba nchini mwenu Saudi Arabia zipo adhaana mbili kwa ajili ya swalah ya ijumaa, jambo ambalo si sahihi. Mambo yalivokuwa ni kwamba imamu anapopanda mimbari ndipo kunaadhiniwa mbele yake adhaana moja. Vitabu vyote vya Sunnah vinasapoti jambo hilo. Naomba unipelekee jambo hili katika mamlaka husika, kama mfano wa Daar-ul-Iftaa´, ambayo inaongozwa na muheshimiwa Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin Baaz ili Allaah aisimamishe haki na aiangamize batili[1].

Jibu: Mambo ni kama alivosema muulizaji kwamba wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kulikuwa na adhaana moja pamoja na Iqaamah. Alipokuwa anapoingia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa ajili ya kutoa Khutbah na swalah basi muadhini anaadhini kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anatoa Khutbah mbili kisha kunasimamwa kwa ajili ya swalah. Hivi ndivo inavotambulika na ndivo ilivokuja katika Sunnah, kama alivosema muulizaji. Ni jambo linalotambulika kwa wanazuoni na waumini. Watu wakawa wengi Madiynah katika zama za kiongozi ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) na ndipo akaona aongeze adhaana ya tatu. Aambiwe kwamba adhaana ya kwanza ni kwa ajili ya kuwazindua watu juu ya kwamba leo ni siku ya ijumaa ili wajiandae na wakimbilie kuswali kabla ya adhaana iliyozoeleka na kutambulika baada ya kupondoka kwa jua na akafuatwa na Maswahabah waliokuweko katika zama zake. Katika zama zake alikuweko ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh), ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf, az-Zubayr bin ´Awwaam na Twalhah bin ´Ubaydillaah (Radhiya Allaahu ´anhum) na wengineo katika Maswahabah vigogo na wakubwa wao. Hivyo waislamu wakawa juu ya hilo katika miji mingi kwa ajili ya kufuata yale yaliyofanywa na kiongozi mwongofu (Radhiya Allaahu ´anh) na pia akafatwa na kiongozi wa nne, ambaye ni ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) na Maswahabah wengineo.

Kinacholengwa ni kwamba haya yamefanywa na kiongozi ´Uthmaan na wa baada yake na wakaendelea juu yake waislamu wengi katika miji na vimbunga mpaka hii leo. Hivo ni kwa ajili ya kufanyia kazi Sunnah hii iliyofanywa na ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) kutokana na Ijtihaad yake na kuwatakia kwake mema waislamu. Hapana vibaya katika hilo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu. Ziumeni kwa magego yenu.”[2]

Naye ni katika makhaliyfah waongofu. Isitoshe manufaa ni yenye kuonekana katika hilo. Kwa ajili hiyo Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wakalichukua na hawakuona lina neno kwa sababu ni miongoni mwa Sunnah za makhaliyfah waongofu ambaye ni ´Uthmaan na ´Aliy na Maswahabah waliokuweko katika zama hizo – Allaah awawie radhi wote.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/347-349).

[2] Abu Daawuud (4607).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 55-57
  • Imechapishwa: 27/11/2021