Swali 16: Mimi nasumbuliwa na kutokwa daima na upepo na natawadha wakati wa kila swalah wakati wa adhaana. Siku ya ijumaa natawadha kabla ya adhaana ya kwanza na natawadha mara myingine baada ya adhaana ya kwanza. Ni ipi hukumu ya kitendo changu hichi[1]?

Jibu: Ambaye hadathi yake ni yenye kudumu, kwa upepo, kutokwa mkojo hovyo na sababu nyenginezo, basi atawadhe kwa ajili ya kila swalah baada ya kuingia wakati wa swalah. Hakimdhuru kitachomtoka katika hadathi katika wakati huohuo au katika swalah hiyohiyo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia ambaye anatokwa na damu ya ugonjwa:

“Tawadha juu ya kila swalah.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake.

Ambaye ana damu ya ugonjwa ni yule ambaye inaendelea kwake damu isiyokuwa damu ya hedhi.

Kwa haya muulizaji anapata kufahamu kwamba ni lazima atawadhe baada ya kuingia wakati wa swalah kwa ambaye hadathi yake ni yenye kudumu.

Akishatawadha kwa ajili ya swalah ya ijumaa saa sita – ambayo ni ile saa kabla ya kupondoka kwa jua – itasihi kufanya hivo. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yanayofahamisha juu ya kusihi kutekeleza swalah ya ijumaa saa sita, nayo ndio maoni ya kikosi cha wanazuoni. Lakini bora ni kuitekeleza baada ya jua kipinduka kwa ajili ya kutendea kazi Hadiyth zote na kutoka nje ya tofauti za  wanazuoni. Kwa sababu wanazuoni wengi wanaona kuwa swalah ya ijumaa haisihi kabla ya jua kupinduka, kama ilivyo swalah ya Dhuhr. Hivyo ni kwa ajili ya kufanyia kazi Hadiyth ambazo zinasema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali swalah ya ijumaa pindi jua linapondoka.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/340-341).

[2] al-Bukhaariy (221), at-Tirmidhiy (116) na Ahmad (23016).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 54-55
  • Imechapishwa: 27/11/2021