Imepokelewa kwamba Sa´iyd bin Jubayr amesema:
“Hakuna yeyote aliyepewa kile walichopewa ummah huu. Allaah (Ta´ala) amesema:
الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ
”Ambao unapowafika msiba basi husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea – hao zitakuwa juu yao baraka kutoka kwa Mola wao na rehema na hao ndio wenye kuongoka.”[1]
Angelikuwa mtu, basi angelipewa Ya´quub (´alayhis-Salaam). Hukusikia pale aliposema:
وَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا أَسَفَىٰ عَلَىٰ يُوسُفَ وَابْيَضَّتْ عَيْنَاهُ مِنَ الْحُزْنِ فَهُوَ كَظِيمٌ
“Na akajitenga nao na akasema: “Ee majonzi yangu juu ya Yuusuf!” na macho yake yakageuka meupe [kwa kulia] kutokana na huzuni naye huku akiwa amezuia ghaidhi.”?[2]
Imepokelewa namna ambavyo mtu mmoja alikuja kwa al-Hasan al-Baswriy (Rahimahu Allaah) akasema:
“Ee Abu Sa´iyd! Nilikuwa na mtoto mdogo akafa. Ninapoona kitu katika alivyokuwa anacheza navyo, basi nahuzunika sana. Naogopa hilo lisije kusababisha kukosa ujira wangu.” Akasema: “Allaah (Ta´ala) hatobatilisha thawabu zako. Unapoona kitu katika hayo basi sema: “Ee Allaah! Mfanye kuwa ni ujira kwangu. Ee Allaah! Mfanye kuwa ni mtangulizi wangu.”
Miongoni mwa yanayotajwa kuhusu subira ya watu waliofiwa na wapenzi wao na tanzia zao nzuri, ni yale yaliyosihi kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye amesema:
“Mmoja katika watoto wa kiume wa Abu Twalhah na Umm Sulaym alifariki. Mke wake akawaambia familia yake: “Msimwambie Abu Twalhah mpaka mimi kwanza nimwambie.” Akaja ambapo akamhudumia chakula cha jioni. Akala na kunywa. Baada ya hapo akajitengeneza vyema kama alivyokuwa akijitengeneza hapo kabla, ambapo akalala naye. Alipoona kuwa amekwishashiba na kuridhika, akasema: “Ee Abu Twalhah! Unaonaje endapo watu watawaazima kitu chao kuwapa familia fulani kisha baadaye wakakitaka kitu chao, je, watu hao wana haki ya kuwakatalia kukirudisha?” Akasema: “Hapana.” Ndipo akasema: “Taraji malipo juu ya mwanao.” Akakasirika na kusema: “Umeniacha mpaka umenichafua kisha ndio unanieleza kuhusu mwanangu?” Akaondoka mpaka akafika kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumweleza yaliyopitika. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Allah akubarikieni juu ya usiku wenu wa jana.” Akashika ujauzito.”[3]
Humo imetajwa namna alivyozaa mtoto wa kiume na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamfuta uso wake na kumpa jina la ´Abdullaah. Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim, ambaye ndiye mwenye tamko hili fupi. Katika upokezi wa al-Bukhaariy Sufyaan bin ´Uyaynah amesema:
“Akasema bwana mmoja katika Answaar: “Nikaona walikuwa na watoto kumi, na wote walikuwa wamehifadhi Qur-aan.” Bi manaa katika watoto wa ´Abdullaah. Kwa msemo mwingine ambao walizaliwa kutokana na lile tendo la ndoa la usiku ule ambao alifariki yule mtoto mlengwa. Mtoto aliyefariki alikuwa akiitwa Abu ´Umayr. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akimtania na kusema:
“Ee Abu ´Umayr! Nughayr amefanyika nini?”[4]
Twaahir bin Muhammad bin al-Haddaad ameongeza ziada mwishoni mwa Hadiyth iliyotajwa katika kitabu chake “´Uyuun-ul-Majaalis” kupitia kwa Mu´aawiyyah bin Qurrah kwa cheni ya wapokezi pungufu. Imekuja mwishoni mwake:
“Akashika ujauzito wa mtoto wa kiume ambaye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akampa jina la ´Abdullaah: “Namuhimidi Allaah ambaye amefanya katika ummah wangu kupatikana mwanamke mwenye subira mno, kama mwanamke wa wana wa israaiyl.” Kukasemwa: “Ee Mtume wa Allaah! Ni zipi zilikuwa khabari zake?” Akasema: “Katika wana wa israaiyl alikuwepo mwanamke na alikuwa na mume. Walikuwa na watoto wawili wa kiume. Mume wake alikuwa amemwamrisha kupika chakula ili awaalike watu kwacho. Akafanya hivo na watu wakakusanyika katika nyumba yake. Wakaondoka wavulana hao wawili wakicheza karibu na wakatumbukia ndani ya kisima cha nyumba hiyo. Akachukia kushawishi ugeni wa mume wake, akawaingiza nyumbani na kuwafunika kwa nguo. Wakati wageni walipoondoka mume wake akaja na kusema: “Wako wapi wavulana wangu wawili?” Akasema: “Wako chumbani.” Mwanamke huyo alikuwa amejipaka manukato na kujionyesha kwa mume wake, mpaka akamjamii. Kisha akasema: “Wako chumbani.” Baba yao akawaita ambapo wakaja. Mwanamke yule akasema: “Allaah ametakasika kutokana na mapungufu! Naapa kwa Allaah! Walikuwa wamekufa. Lakini Allaah (Ta´ala) amewahuisha hali ya kuwa ni malipo ya subira yangu.”
Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) watoto wake walikuwa hawaishi. Wakati alipoambiwa kuwa watoto wake hawaeshi, akasema:
“Namshukuru Allaah ambaye anawachukua kwenda kuwahifadhi katika maisha ya milele.”[5]
[1] 2:155-157
[2] 12:84
[3] Muslim (2150).
[4] al-Bukhaariy katika “al-Adab al-Mufrad” (269).
[5] Geni kwa mujibu wa as-Sakhaawiy katika “Irtiyaah-ul-Akbaad”.
- Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
- Mfasiri: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 85-89
- Imechapishwa: 16/08/2023
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)