15. Cha kusema baada ya kupatwa na msiba na mtihani

Yule aliyefikwa na msiba, au aina yoyote ya mtihani, anatakiwa kusema:

إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ

“Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.”

Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hakuna muislamu yeyote anayepatwa na msiba na akasema:

إِنَّا لله وإِنَّا إِلَيْه راجعونَ اللهُمَّ أَجِرْني في مُصِيبَتي وَأَخْلِفْ لي خَيْراً منها

”Hakika sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea. Ee Allaah! Nilipe kwa msiba wangu na Unipe badala yake kheri kuliko hiyo.”

isipokuwa humlipa kwa msiba wake na humpa badala ilio bora kuliko hiyo.” Wakati Abu Salamah alipofariki, nikasema: ”Ni muislamu yupi bora kuliko Abu Salamah? Nyumba yake ndio ilikuwa ya kwanza kuhajiri kwenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Kisha nikasema namna hiyo – na Allaah akanipa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[1]

Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mmoja wenu akifikwa na msiba basi, na aseme:

إنا لله وإنا إليه راجعون ، اللهم عندَك أَحتَسِبُ مُصيبَتي ، فأَجِرْني فيها ، وأَبدِلْني بها خيرًا منها

”Hakika sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea. Ee Allaah! Hakika Kwako ndio nataraji malipo ya msiba wangu. Nilipe kwao na nibadilishie bora kuliko wenyewe.”[2]

Imekuja kwa Ahmad:

“Hakuna muislamu yeyote anayefikwa na msiba na akaukumbuka, hata kama utakuwa wa zamani, akasema: “Hakika sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea”, isipokuwa Allaah (Ta´ala) atamfanyia upya wakati huo na kumpa mfano wa ujira wake siku ile ulipompata.”[3]

Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kupiga kwenye mapaja kunabatilisha ujira. Subira huzingatiwa pale mwanzoni mwa pigo. Ukubwa wa thawabu inakuwa kwa kiasi cha ukubwa wa msiba. Yule mwenye kusema “Hakika sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea” baada ya msiba wake, basi Allaah huyafanya upya malipo yake kama siku ile ulipompata.”

Allaah (Ta´ala) amesema:

الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

”Ambao unapowafika msiba basi husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea – hao zitakuwa juu yao baraka kutoka kwa Mola wao na rehema na hao ndio wenye kuongoka.”[4]

´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Ni uzuri gani wa mizani miwili! Ni uzuri gani wa ziada!”[5]

Mutwarrif bin ´Abdillaah bin ´Abdillaah bin ash-Shikhkhiyr amesema baada ya kufariki mwanae:

“Naapa kwa Allaah! Lau ningelikuwa na ulimwengu mzima na vyote vilivyomo ndani yake, ambapo Allaah akavichukua kutoka kwangu na kuniahidi kunywa maji kama malipo, basi ningeona hicho nilichobadilishiwa kuwa ni haki kabisa. Tusemeje juu ya swalah, rehema na uongofu?”

Thaabit al-Bunaaniy amesimulia kwamba wakati ´Abdullaah bin Mutwarrif alipofariki, basi Mutwarrif aliwatokea watu akiwa amevaa vizuri na amejipaka mafuta. Watu walipomuona namna hiyo wakakasirika na kusema:

“´Abdullaah amekufa na wewe unatoka ukiwa umevaa namna hiyo na mafuta?” Akajibu: “Je, nijichimbie shimo kwa ajili ya jambo hilo ilihali Mola wangu ameniahidi zawadi juu ya jambo hilo – na kila zawadi ni yenye kupendeza zaidi kwangu kuliko dunia na vyote vilivyomo ndani yake? Allaah (Ta´ala) amesema:

الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

”Wabashirie wale wenye kusubiri ambao unapowafika msiba basi husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea – hao zitakuwa juu yao baraka kutoka kwa Mola wao na rehema na hao ndio wenye kuongoka.”[6]

Je, nijichimbie shimo kwa ajili ya jambo hilo baada ya haya?”[7]

[1] Muslim (918).

[2] Abu Daawuud (3119), at-Tirmidhiy (3512), an-Nasaa’iy (6/81) na Ibn Maajah (1598). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (3119).

[3] Ahmad (1734) na Ibn Maajah (1600). Dhaifu mno kwa mujibu wa Ahmad Shaakir na al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf Sunan Ibn Maajah” (312).

[4] 2:155-157

[5] Ameipokea al-Bukhaariy kwa cheni ya wapokezi pungufu.

[6] 2:155-157

[7] az-Zuhd, uk. 245, ya Ahmad bin Hanbal.