al-Mu´aafaa bin ´Imraan amesimulia kutoka kwa Shihaab bin Khiraash, kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin Ghanm, ambaye amesema:
“Tuliingia kwa Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye alikuwa amekaa karibu na kichwa cha mwanawe. Mtoto huyo alikuwa katika hali ya kukata roho. Hatukuweza kujizuia kutokwa na machozi. Baadhi yetu tukaomboleza, ambapo Mu´aadh akatukemea na kusema: “Acha! Naapa kwa Allaah! Allaah anajua kuwa naridhia jambo hili zaidi kuliko vita vyote nilivyopigana bega kwa bega pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwani hakika mimi nimemsikia akisema: “Yule mwenye mtoto wa kiume anayempenda na akasubiri juu ya msiba wake na akataraji thawabu, basi Allaah atambadilishia yule maiti nyumba bora kuliko nyumba yake na matulizo bora kuliko matulizo yake, na atambadilishia yule aliyefikwa na msiba sifa, rehema, msamaha na ridhaa. Hakukupita kitambo kirefu mtoto yule akafariki wakati ambapo muadhini alipoadhini kwa ajili ya swalah ya Dhuhr. Tukaenda kwa ajili ya kuswali. Wakati tuliporudi tukakuta ameshamuosha, amempaka dawa na kumvika sanda. Bwana mmoja akaja na machela yake. Hakukusubiriwa ushahidi wa ndugu wala mkusanyiko wa majirani. Pindi tulipopata khabari hiyo tukalifuata na kusema: “Allaah akusamehe, ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Kwa nini husubiri mpaka basi angalau tumalize swalah zetu na tuhudhurie kwa mwana wa ndugu yetu?” Akasema: “Tumeamrishwa tusisubiri kitambo baada ya kufa kwa jamaa zetu, ni mamoja mchana au usiku. Kufanya matangazo juu yao ni miongoni mwa mambo ya kipindi kabla ya kuja Uislamu.” Akashuka ndani ya kaburi na mwingine akashuka pamoja naye. Nikasema: “Mtu wa tatu, ee Abu ´Abdir-Rahmaan?” Akasema: “Wanasema mtu wa tatu wale wasiojua.” Baada ya kulifukia kaburi udongo na akataka kutoka, nikamnyooshea mkono wangu kumsaidia kutoka nje ya kaburi. Akakataa na akasema: “Sikukatalii kwa sababu nina nguvu, lakini ni kwa sababu sipendi mjinga aone kuwa nimefanya hivo kwa sababu ya kukata tamaa kwangu tamaa na changamoto kwa ajili ya msiba wangu.” Kisha akaenda katika kikao chake, akaomba mafuta na kujipaka mafuta, akaomba wanja na kujipaka wanja na akaomba koti akalivaa. Siku hiyo alitabasamu mara kwa mara akimaanisha anachomaanisha. Kisha akasema: “Hakika sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea. Allaah atawafanya wote waliokufa wafuatiwe na wengine, kila msiba ufuatiwe na rambirambi na kukidiriki kila kilichopita.”
Naafiy´, mtumwa wa ´Umar aliyemwacha huru, ameeleza:
“Mmoja katika watoto wa ´Abdillaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliumwa, ambapo akamsikitikia mno mpaka wakasema baadhi ya watu: “Tunachelea juu ya mzee huyu endapo kutatokea jambo juu ya mtoto huyu.” Kijana yule akafariki. Ibn ´Umar akatoka kwenda katika mazishi yake, na hakukuwepo na mtu ambaye inaonekana kwake furaha kama yeye. Akaulizwa juu ya jambo hilo, ambapo akasema: “Hakika hapana vyenginevyo hiyo ni rehema Kwake. Wakati ilipotekelezeka amri ya Allaah, tukairidhia.”[1]
[1] ar-Ridhwaa ´an-il-Laah wa Qadhwaa-ih (98) ya Ibn Abiyd-Dunyaa.
- Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
- Mfasiri: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 89-91
- Imechapishwa: 16/08/2023
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)