16. Radd juu ya utata wa kwamba Ummah huu hauwezi kufanya shirki

Nne: Miongoni mwa

shubuha zao ni kwamba katika Ummah huu wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwezi kutokea shirki na kwamba eti wao wanasema “hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah” na kwamba yale wanayofanya pamoja na mawalii na waja wema kwenye makaburi yao sio shirki. Jibu juu ya utata huu ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa kutatokea katika Ummah huu kujifananisha na mayahudi na manaswara katika yale waliyomo. Katika jumla ya mambo hayo ni kuwafanya wanavyuoni wa kiyahudi na watawa kuwa ni waungu badala ya Allaah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mtafuata mienendo na yale waliyokuwa kabla yenu hatua kwa hatua kiasi cha kwamba mpaka wakiingia shimo la mburukenge nanyi mtaingia.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Unamaanisha mayahudi na manaswara?” Akasema: “Kina nani wengine?”[1]

Hivyo akaeleza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba Ummah huu utaiga yaleyale yaliyofanywa na nyumati zilizotangulia katika mambo ya dini, desturi na siasa. Shirki ilipatikana katika nyumati zilizotangulia na vivyo hivyo shirki imepatikana katika Ummah huu. Yametokea yale aliyoelezea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yako makaburi yanayoabudiwa badala ya Allaah kwa kufanyiwa aina mbalimbali za ´ibaadah.

Vilevile ameeleza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba:

“Qiyaamah hakitosimama mpaka wawepo waliohai katika Ummah wangu ambao watajiunga pamoja na washirikina na mpaka kundi katika Ummah wangu waabudu mizimu.”[2]

Ameipokea Abu Daawuud na Ibn Maajah.

Kumetokea katika Ummah huu shirki, misingi angamivu na makundi potofu ambayo mengi yametoka katika Uislamu.

[1] al-Bukhaariy (13/300) pamoja na ”al-Fath”.

[2] Abu Daawuud (4252).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 28-29
  • Imechapishwa: 27/03/2019