16. Ngome ya waislamu kabla ya siku ya Qiyaamah

113- Abud-Dardaa´ ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kambi ya waislamu siku ya Kichinjwa itakuwa al-Ghutwah karibu na mji wa Dameski ambao ndio mji bora wa Shaam.”[1]

Ameipokea Abu Daawuud, at-Twabaraaniy ameipokea kwa matamshi:

“Wakati huo ndio itakuwa sehemu bora ya kuishi… “

al-Haakim ameipokea kwa matamshi:

“Kipindi hicho ndiko itakuwa sehemu bora ya waislamu kuishi… “

Ibraahiym al-Junayd amesema:

“Nimemsikia Yahyaa bin Ma´iyn akiulizwa juu ya Hadiyth kuhusu kichinjwa cha rumi. Akasema: “Hakuna Hadiyth yoyote iliyopokelewa na watu wa Shaam ilio Swahiyh kama Hadiyth ya Swadaqah bin Khaalid.”

Bi maana Hadiyth ya Abud-Dardaa´ aliyopokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kambi ya waislamu siku ya Kichinjwa itakuwa al-Ghutwah karibu na mji wa Dameski ambao ndio mji bora wa Shaam.”

114- Ka´b-ul-Ahbaar amesema:

“Ngome ya waislamu wakati wa kichinjwa ni Dameski. Ngome yao dhidi ya ad-Dajjaal ni mto wa Jordan. Ngome yao dhidi ya Ya´juuj na Ma´juuj ni Twuur.”

115- al-Awzaa´iy amesema:

“Nimefikiwa na khabari ya kwamba Shaam kuna bonde linaloitwa al-Ghuutwah. Huko kuna mji unaoitwa Dameski na ndio itakuwa mji bora kabisa wa Shaam wakati wa Kichinjwa.”

116- ´Abdullaah bin Salaam amesema:

“Mwisho wa zama Dameski ndio itakuwa ngome ya waislamu kutokamana na Kichinjwa.”

117- ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw akisema:

“Nakutamania kile ninachojitamania nafsi yangu na watoto wangu; Shikamana na Dameski.”

118- ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw akisema:

“Sikupendelea kuishi Misri na hazini zake baada ya 150. Dameski ni bora lau wangelikuwa wanajua.”

119- Ibn Muhayriyz ameeleza kuwa Ruwayfiy´ bin Thaabit al-Answaariy (Radhiya Allaahu ´anh) – ambaye alimpa kiapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) chini ya mti – alimwambia:

“Ishi Palestina maadamu waarabu watakuwa wakingali wazuri. Pindi watapoanza kuita kama walivyokuwa wakifanya katika kipindi cha kishirikina basi hama kwenda Dameski – na mashariki yake ni bora kuliko sehemu zengine.”

120- Mak-huul amesema:

“Warumi watapora Shaam kwa masiku arubaini. Miji itayosalimika tu ni Dameski na ´Ammaan.”

121- Abul-A´yas ´Abdur-Rahmaan bin Salmaan amesema:

“Atakuja mfalme wa kigeni kutoka nje na atashinda juu ya miji yote isipokuwa tu Dameski.”

122- ´Abdus-Salaam at-Tanuukhiy amesema:

“Wanachuoni wetu wametueleza pindi walipoufungua mji wa Dameski wakati wa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) walipata jiwe lililokuwa limeandikwa kwa maandishi ya kigiriki. Hivyo wakamleta mwanamme wa kigiriki kulisoma. Kulikuwa yafuatayo:

“Dameski ni jabari. Hakuna jabari yeyote anayekusudia kuivamia isipokuwa Allaah humvunja. Majabari wanajenga na nyani zinaharibu. Hawa wa mwisho waliyotajwa ni waovu zaidi mpaka siku ya Qiyaamah.”

[1] Abu Daawuud (4298), Ahmad (57197), at-Twabaraaniy katika ”al-Awsat” (3205) na al-Haakim (4/486).

  • Mhusika: Imaam ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Baghdaadiy al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-ush-Shaam, uk. 127-136
  • Imechapishwa: 10/02/2017